WAZIRI
MKUU Kassim Majaliwa ameuagiza uongozi wa Jeshi la Magereza nchini
ukamilishe mkakati wa ujenzi wa magereza za wilaya kwa wilaya zisizokuwa
na magereza.
Ametoa
agizo hilo leo (Jumatatu, Juni 3, 2019) wakati akifungua Gereza la
wilaya ya Ruangwa mkoani Lindi. Uzinduzi huo umefanyika kwenye viwanja
vya gereza hilo.
Waziri
Mkuu amesema uwepo wa magereza katika wilaya zote nchini utasaidia
kumaliza tatizo la msongamano wa wafungwa na mahabusu kwenye magereza ya
jirani.
“Kutokuwepo
kwa magereza ya wilaya kunasababisha msongamano wa wafungwa na mahabusu
katika magereza ya jirani, pamoja na kuchelewesha upatikanaji wa haki.”
Waziri
Mkuu amesema kwamba ufunguzi wa gereza la Ruangwa utatatua tatizo la
msongamano wa wafungwa na mahabusu katika Gereza la wilaya ya
Nachingwea
Awali
wakazi wa wilaya hiyo waliokabiliwa na tuhuma mbalimbali au
waliohukumiwa vifungo walikuwa wakipelekwa katika Gereza la wilaya ya
Nachingwea.
Amesema
kitendo cha kupelekwa Nachingwea kilikuwa kikiwanyima wafungwa na
mahabusu fursa ya kuonana na ndugu au mawakili wao kutokana na umbali
uliokuwepo.
“Mbali
na ndugu na jamaa kushindwa kwenda kuwaona ndugu zao pia Jeshi la
Polisi lilikuwa likilaumiwa kuwa linawachelewesha mahubusu kuja
kusikiliza mashauri yao.”
Waziri
Mkuu amesema uwepo wa gereza hilo katika wilaya ya Ruangwa umeipunguzia
Serikali gharama za kuwasafirisha mahabusu na wafungwa kwenda
Nachingwea.
Awali, Waziri waMambo
ya Ndani ya Nchi, Kangi Lugola amesema Gereza la Wilaya ya Ruangwa ni
nyenzo muhimu katika kuimarisha ulinzi na usalama wa wilaya hiyo.
Amesema
gereza hilo ni chachu ya kuimarika kwa uchumi wa wilaya hiyo kwa
kupitia sekta ya kilimo kwani kutakuwa na kambi za kilimo, hivyo
wananchi nao watajifunza.
“Wananchi
msilione gereza hili kama adui kwenu, halijaja kuwafunga bali lipo kwa
ajili ya kuimarisha amani, ulinzi na usalama wa wilaya yetu pamoja na
kutoa elimu mbalimbali.”
Kwa upande wake,
Kamishna Jenerali wa Magereza Phaustine Kasike amesema ujenzi huo
umefanywa na kikosi cha ujenzi cha Magereza kwa kutumia nguvukazi ya
wafungwa.
Amesema
awamu ya kwanza ya ujenzi wa gereza hilo imekamilika na imegharimu sh.
bilioni 1.5 hivyo umekamilisha uwepo wa magereza katika wilaya zote za
mkoa wa Lindi.
Kamishna
huyo amesema ujenzi huo ungefanywa na mkandarasi wa nje ungegharimu sh.
bilioni 2.226, hivyo kwa kutumia kikosi cha Magereza wameokoa sh.
milioni 635.675.
Amesema
kwa sasa gereza hilo lina uwezo wa kuwahifadhi wahalifu 250 hadi 280 na
likikamilika itakuwa na uwezo wa kuwahifadhi wahalifu 500.
Kamishna
Kasike amesema gereza hilo lina ardhi yenye ukubwa wa ekari 80, ambapo
ekari saba zitatumika kwa ajili ya majengo ya gereza, maegezo ya magari
na karakana.
“Ekari
56 zitatumika kwa ajili ya ujenzi wa nyumba 100 za makazi, ekari sita
ujenzi wa majengo ya huduma kama zahanati na ekari nane zitatumika
katika kilimo cha bustani.”
Baadhi
ya wananchi waliohudhuria ufunguzi huo wameishukuru Serikali ya Awamu
ya Tano inayoongozwa na Rais Dkt. John Magufuli kwa kuboresha huduma za
jamii.
Mmoja
wa wananchi hao Zena Selemani amesema kabla ya ujenzi wa gereza hilo
walikuwa wanashindwa kuwatembelea ndugu zao walofungwa katika gereza la
Nachingwea.
(mwisho)
EmoticonEmoticon
Note: Only a member of this blog may post a comment.