WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa ameagiza halmashauri zote za majiji na miji zihakikishe kuwa kuanzia sasa zinatenga maeneo ya michezo na burudani kila zinapopima viwanja.
“Naagiza
 kuanzia sasa, maeneo yote yanayopimwa na halmashauri na miji yote 
nchini, lazima yazingatie uwepo wa maeneo ya michezo na burudani,” 
amesisitiza Waziri Mkuu.
Waziri Mkuu ametoa agizo hilo leo (Jumatatu, Juni 10, 2019)wakati akifungua mashindano ya Umoja wa Michezo na Taaluma kwa shule za msingi na sekondari Tanzania, katika Uwanja waNangwanda Sijaona mkoani Mtwara. Zaidi ya wanafunzi 5,400 wanashiriki mashindano hayo.
Pia,
 amezitaka Halmashauri ziweke mpango madhubuti wa kuyaendeleza maeneo ya
 michezo na burudani sambamba na miundombinu inayozingatia mahitaji ya 
wote bila kubagua.
Amesema
 katika baadhi ya maeneo kumekuwepo na uhaba wa viwanja vya michezo kwa 
sababu ya mipango miji isiyozingatia mipango endelevu ya sekta 
mbalimbali.
Hivyo,
 Waziri Mkuu ameagiza yafanyike marekebisho na hatua za haraka ili kutoa
 fursa ya ukuaji wa michezo na kusaidia wananchi kushiriki michezo, 
mazoezi na kupata burudani.
Amesema
 ifikapo Septemba 30, 2019, kila halmashauri iwe imefanya mapitio ya 
maeneo yote yaliyokuwa yamepimwa kwa matumizi ya huduma maalum ikiwemo 
michezo, burudani, shule na ibada na kutoa taarifa kama yanatumika kwa 
ajili hiyo au vinginevyo.
Wakati huo huo,Waziri
 Mkuu ameiagiza Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia irudishe na 
iimarishe mchepuo wa Elimu kwa Michezo Chuo cha Ualimu Butimba ili 
kupata wataalam zaidi. 
“Halmashauri
 ziendelee kuwaruhusu walimu mbalimbali nchini kuhudhuria mafunzo ya 
michezo katika chuo cha Mendeleo ya Michezo Malya ili kupunguza uhaba wa
 watalaam wa michezo katika shule mbalimbali na nchini kwa ujumla.”
Waziri
 Mkuu amesema michezo ni muhimu kwa wanafunzi kwa kuwa itawaepusha 
vijana na makundi yasiyofaa yakiwemo matumizi ya dawa za kulevya na 
vitendo vingine visivyoendana na maadili ya Kitanzania.
Amesema
 michezo itawawezesha vijana kuwa na afya bora na kufanya vema katika 
masomo yao kwa kuwa ili waweze kusoma vema ni sharti afya zao ziwe 
njema. Pia sanaa itasaidia katika kuutambulisha utamaduni wetu ndani na nje ya mipaka ya nchi yetu. 
“Kwa
 hiyo, ni vema tukatambua kuwa michezo na sanaa ni sehemu ya elimu bora.
 Hivyo, ni muhimu kutekeleza dhana ya elimu ya michezo ili tuweze 
kufikia maendeleo tarajiwa.”
 Kadhalika,
 Waziri Mkuu amesema sambamba na michezo iliyozoeleka, pia wanaweza 
kuibua michezo yao ya asili ambayo itautambulisha utamaduni wetu. “Nitoe
 wito kwa shule zetu, ziendeleze ubunifu wa kuibua vipaji vya sanaa na 
michezo ya asili katika maeneo yetu kwa lengo la kuenzi utamaduni wetu.”
Akizungumzia kuhusu mashindano ya mwaka huu ambayo yameshirikisha wanafunzi
 wengi zaidi wenye mahitaji maalumu, Waziri Mkuu amesema waendelee 
kuwahusisha wanafunzi wote katika michezo, sanaa na burudani bila kujali
 aina ya ulemavu walionao. 
Amesema jambo hilo ni muhimu kwa kuwa vipaji vipo kwa wote na fursa ndizo zitakazowawezesha kuonesha vipaji hivyo na kuvikuza.
Waziri
 Mkuu amewasisitiza wadau wote wa shule za msingi, sekondari, vyuo, 
sehemu za kazi na wizara, waweke mipango ya kudumu ya kuwashirikisha 
watu wenye mahitaji maalumu katika shughuli mbalimbali za kijamii na 
kiuchumi bila ubaguzi wowote. 
“Hakikisheni
 baadhi ya vikwazo katika kushirikisha watu wenye mahitaji maalumu 
kwenye michezo vinaondolewa. Vikwazo hivyo ni pamoja na kutokuwepo kwa 
mipango endelevu katika maeneo mbalimbali na uwepo wa mitazamo hasi ya 
baadhi ya walimu, wazazi na viongozi katika maeneo yao dhidi ya uwezo wa
 wanafunzi wenye mahitaji maalum.”
Aidha,
 Waziri Mkuu ametuamia fursa hiyo kuupongeza Mkoa wa Simiyu kwa kuwa 
mmoja kati ya Mikoa ya mfano katika kutekeleza agizo lake la mwaka jana 
alilolitoa kupitia michezo hiyo la kuanzishwa kwa shule maalumu za 
michezo.
Mkoa
 wa Simiyu umejenga Shule ya Sekondari itakayokuwa kituo cha kukuza 
vipaji vya wanafunzi katika michezo. “Naagiza mwakani wanafunzi wote 
walioonesha vipaji katika michezo watakaofaulu Mtihani wa Elimu ya 
Msingi wapangwe katika shule hiyo ili wakakuze vipaji vyao.” 
Amesema
 bila ya kuwa na mipango ya kulea na kukuza vipaji kutoka ngazi za chini
 Taifa haliwezi kupata mafanikio katika michezo nchini. Kwani katika 
kipindi ambapo michezo hiyo ilisitishwa kiwango cha michezo ya aina 
mbalimbali kilikuwa chini sana.
“Tangu
 tumerejesha shughuli za michezo katika shule zetu tumekuwa na mafanikio
 makubwa sana ikiwemo kupata wachezaji wanaofuzu kucheza soka la kulipwa
 kwenye viwango vya kimataifa kama Mbwana Samatta (Genk –Belgium), Simon
 Msuva (Difaa El Jadid – Morocco), “
Wengine
 ni Shiza Kichuya (Enppi –Misri), Thomas Ulimwengu (JS Saoura – 
Algeria), Hamid Mao (Petrojet – Misri), Adi Yusuph (Blackpool –England),
 Hassan Kessy (Nkana – Zambia), Yahya Zaydi (Ismaily –Misri), Shabani 
Chilunda, (Tenerife – Hispania) Rashid Mandawa (BDF- Botswana), Farid 
Mussa ( Tenerife– Hispania).
Waziri
 Mkuu amesema pamoja na mafanikio yaliyopatikana, jitihada zaidi 
zinahitajika ili kuwa na maendeleo ya kutosha katika shughuli za michezo
 nchini.
Hivyo,
 Waziri Mkuu ameitaka Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo kwa 
kushirikiana na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia na Ofisi ya Rais 
TAMISEMI wakamilishe tathmini ya shule 56 za Serikali zilizokuwa 
zimetengwa kwa ajili ya kuendeleza vipaji vya michezo.
Ufunguzi
 huo umehudhuriwa na Waziri wa Nchi OR-TAMISEMI, Selemani Jafo, Waziri 
wa Elimu Sayansi na Teknolojia, Profesa Joyce Ndalichako, Naibu Waziri 
wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Juliana Shonza, Maafisa Elimu 
kutoka mikoa yote nchini, walimu wa michezo pamoja na Maofisa wengine wa
 Serikali. 
EmoticonEmoticon
Note: Only a member of this blog may post a comment.