Sunday, June 16, 2019

WAZIRI MKUU AWASHAURI WATANZANIA KUJIWEKEA AKIBA KUPITIA HISA


WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema ni wakati muafaka kwa Watanzania kuanza kujiwekea akiba kwa kununua hisa kupitia taasisi za kifedha nchini ikiwemo benki ya CRDB.

Ametoa kauli hiyo leo (Jumapili, Juni 16, 2019) wakati wa bonanza kati ya Wabunge na watumishi wa benki ya CRDB lililofanyika kwenye uwanja wa Jamhuri jijini Dodoma.

Waziri Mkuu amesema suala la wananchi kujiwekea akiba ni muhimu kwa ajili ya maendeleo yao. "Nashauri wananchi tutumie taasisi za fedha kujiwekea akiba pamoja na kukopa mikopo kwa ajili ya maendeleo yetu."

Akizungumzia kuhusu bonanza hilo lililoandaliwa na benki ya CRDB, Waziri Mkuu amesema michezo ni sehemu nzuri kujenga afya, furaha na kujenga mshikamano wa karibu baina ya benki hiyo na wananchi ambao ni wateja.

Michezo iliyochezwa katika bonanza hilo ni mpira wa miguu ambapo timu ya CRDB ilishinda baada ya kuifunga timu ya Bunge penati tatu kwa moja na kwa upande wa mchezo wa mpira wa pete timu ya Bunge iliibuka na ushindi baada ya kuibugiza CRDB magoli 35 kwa mawili.

Katika mchezo wa kuvuta kamba timu ya Wabunge Wanawake na Wanaume waliibuka na ushindi baada ya kuzishinda timu za CRDB. Upande wa mchezo wa basketball timu ya Bunge ilishinda vikapu 53 kwa 51.


(mwisho)


EmoticonEmoticon

Note: Only a member of this blog may post a comment.