Thursday, July 20, 2017

TUTATEKELEZA AHADI ZOTE ZILIZOTOLEWA NA RAIS-MAJALIWA

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amewahakikishia wananchi kwamba ahadi zote zilizotolewa na Rais Dkt. John Magufuli katika maeneo mbalimbali nchini zitatekelezwa, hivyo amewaomba waendelee kuiamini na kushirikiana na Serikali yao.

Ametoa kauli hiyo jana jioni (Alhamisi, Julai 20, 2017) wakati akizungumza na wananchi wa wilaya ya Songwe kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika katika uwanja wa Mkuwajuni.Waziri Mkuu yuko Mkoani Songwe kwa ziara ya kikazi.

Waziri Mkuu alisema kwamba Serikali ya awamu ya Tano ipo makini na imejipanga vizuri katika kutekeleza ahadi mbalimbali zilizotolewa na Rais Dkt. Magufuli kama Ilani ya uchaguzi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) ya mwaka 2015-2020 inavyoelekeza.

Waziri Mkuu aliyasema hayo baada ya mbunge wa jimbo la Songwe, Mheshimiwa Philipo Mulugo kumuomba awasaidie kumkumbusha Rais Dkt. Magufuli kuhusu ahadi yake ya ujenzi wa barabara ya lami yenye urefu wa kilomita nne wilayani Songwe.

“Ahadi zote zilizotolewa na Mheshimiwa Rais Dkt. Magufuli tutazitekeleza, ikiwemo na hii aliyoikumbusha Mheshimiwa Mulugo ya ujenzi wa kilomita nne za barabara ya lami. Tunawaomba wananchi muendelee kuwa na imani na Serikali yenu.”

Pia Waziri Mkuu alipiga marufuku wananchi kufanya shughuli za kibinadamu ndani ya mita 60 kutoka katika vyanzo vya maji na kuwataka washirikiane katika utunzaji wa mazingira ili kuliepusha Taifa kugeuka jangwa.

 Alisema ni vema wananchi wakazingatia Sheria ya Mazingira inayozuia kufanya shughuli za kibinadamu zikiwemo za kilimo kwenye maeneo yote ya vyanzo vya maji ndani ya mita 60. Aliwaagiza Wakuu wa Idara kusimamia jambo hilo.

Waziri Mkuu alisema kwa sasa maeneo mengi yanakabiliwa na changamoto ya upatikanaji wa maji jambo ambalo linachangiwa na vitendo vya uharibifu wa mazingira vinavyofanywa na baadhi ya wananchi, hivyo aliwataka wabadilike.

Hata hivyo, alisema Serikali inaendelea na utekelezaji wa Kampeni ya Rais Dkt. Magufuli ya kumtua mama ndoo kichwani, ambapo itahakikisha kwamba wananchi wote wanapata huduma ya maji katika umbali usiozidi mita 400 kutoka kwenye makazi yao.
Pia Waziri Mkuu aliwaeleza wananchi hao kwamba, Serikali bado inaendelea kutafuta vyanzo mbalimbali vya maji na kuhakikisha vinabainishwa na kufanyiwa tathmini ili viweze kuendelezwa na kuongeza upatikanaji wa maji nchini.
Naye Mkuu wa Mkoa wa Songwe, Bi. Chiku Gallawa akizungumzia hali ya upatikanaji wa maji katika mkoa huo alisema watu wanaopata huduma za maji safi na salama katika maeneo ya mijini ni asilimia 42 na vijijini ni asilimia 41.6.
Alisema katika bajeti ya 2017/2018 halmashauri za mkoa huo zimetengewa jumla ya sh bilioni 7.5 kwa ajili ya utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maji ikiwa ni pamoja na ujenzi wa matanki ya kuvunia maji ya mvua katika majengo yaTaasisi za Umma.

Pia mkoa huo unatekeleza mpango kazi wa usambazaji maji katika maeneo ya mijini na vijijini kwa kupanua mifumo ya usambazaji na kuzijengea uwezo mamlaka za maji na ifikapo Desemba mwaka huu wataongeza idadi ya wananchi wanaopata huduma hiyo kutoka asilimia 45.04 hadi asilimia 55.63.


EmoticonEmoticon

Note: Only a member of this blog may post a comment.