*Asema vilivyo mbali na gridi kufungwa
sola
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema hakuna kijiji nchini
kitakachoachwa bila ya kuunganishiwa umeme katika awamu ya tatu ya Mradi wa Nishati
Vijijini (REA).
Amesema Serikali imetenga shilingi trilioni moja kwa
ajili ya kusambaza umeme katika vijiji 8,000 ambavyo bado havijaunganishiwa
nishati hiyo.
Waziri Mkuu alitoa kauli hiyo jana jioni (Jumanne, Julai
11, 2017) alipozungumza kwa nyakati tofauti na wananchi wa wilaya ya Ruangwa.
Waziri Mkuu ambaye ameambatana na mkewe Mama Mary
Majaliwa aliyasema hayo katika mikutano aliyoifanya kwenye vijiji vya Chiapi, Nandanga,
Mbecha na Luchelegwa, ikiwa ni siku ya pili ya ziara yake ya kikazi ya siku nne
Mkoani Lindi.
“Rais wetu Dkt. John Magufuli anajali sana wananchi wake,
hivyo ametenga fedha nyingi zitakazotosheleza kusambaza umeme katika vijiji
vyote vikiwemo na wilaya ya Ruangwa. Gharama za kuunganishiwa umeme huo ni sh.
27,000 tu.”
Pia Waziri Mkuu amesema
mwananchi hawatowajibika tena katika kulipia nguzo wala fomu za maombi
ya kuunganishiwa umeme, kwa sababu tayari gharama hizo zimeshabebwa na Serikali.
Waziri Mkuu
aliongeza kwamba lengo la Serikali ni
kufikisha umeme kwenye vijiji vyote Tanzania na kwa vile ambavyo viko kwenye
maeneo yaliyo mbali na gridi vitafungiwa sola, jambo ambalo litafungua fursa za
ajira na kukuza uchumi.
Waziri Mkuu alisema huduma hiyo ni muhimu kwani mbali ya kutumiwa
majumbani lakini pia kwa kusogezwa karibu na maeneo ya pembezoni
itawezesha zahanati,shule ,viwanda na vituo vya afya kuwa na umeme.
Kwa upande wake Meneja wa Tanesco Mkoa wa Lindi Mhandisi,
Johnson Mwigune alimuhakikishia Waziri
Mkuu kwamba hadi kufikia mwishoni mwa mwezi huu mkandarasi aliyepangiwa katika
vijiji hivyo atakuwa tayari ameanza kazi ya kusambaza umeme.
EmoticonEmoticon
Note: Only a member of this blog may post a comment.