Saturday, July 15, 2017

WATANZANIA KUACHANA NA NGUO ZA MITUMBA-MAJALIWA

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema safari ya Watanzania kuachana na nguo za mitumba imewadia kutokana na uwepo wa viwanda vya kutengeneza nguo nchini.

Pia amesema uwepo wa viwanda hivyo utasaidia wakulima wa pamba kupata soko la uhakika hivyo amewataka walime pamba ya kutosha ili viwanda vipate malighafi.

Waziri Mkuu alitoa kauli hiyo  jana (Jumamosi, Julai 15, 2017) wakati alipotembelea kiwanda cha nyuzi cha Namera kilichoko Gongo la Mboto na kiwanda cha nguo cha Nida kilichopo Ubungo Dar Es Salaam.

Alisema viwanda vya kutengeneza nguo nchini ni ushahidi tosha kwamba nchi iko njiani kuondokana na matumizi ya nguo za mitumba kwa kuwa nguo nyingi zitakuwa zinatengenezwa nchini, hivyo kupatikana kwa bei nafuu.

Alisema kwa sasa wanunuzi wa pamba hawana sababu ya kwenda kuuza nje ya nchi na badala yake wauze katika viwanda vya ndani ili vizalishe nguo za kutosha zitakazouzwa nchini kwa gharama nafuu.

“Pamba yote inaweza kuchakatwa nchini, hivyo hakuna haja ya kuiuza nje ya nchi. Natoa wito kwa wakulima wetu wa pamba walime mazao ya kutosha kwa sababu soko la uhakika ipo na hii ndio safari ya mwisho ya mitumba.”

Awali Waziri Mkuu alitembelea kiwanda cha saruji cha Lake kinachozalisha saruji ya nyati ambapo aliwapongeza wawekezaji wote nchini kwa kuunga mkono jitihada za Rais Dkt. John Magufuli za kuifanya Tanzania kuwa ya uchumi wa viwanda.

Katika kiwanda hicho ambacho kinazalisha tani 700,000 kwa mwaka kimeajiri watu 2000 na kinalipa kodi ya  sh. bilioni 81.312 kwa mwaka, Waziri Mkuu aliwataka watumishi wake wawe waaminifu, wafanye kazi kwa weledi na wawe waadilifu.

Pia Waziti Mkuu alitoa wito kwa wamiliki wa viwanda vyote nchini kuhakikisha wanatoa kipaumbele cha ajira kwa wananchi waishio katika maeneo ya karibu na viwanda sambamba na kulipa kodi kwa wakati na kwa viwango sahihi. 


EmoticonEmoticon

Note: Only a member of this blog may post a comment.