*Azindua Wakala wa Barabara Vijijini na Mijini
*Asema utashusha bei ya vyakula mijini
CHANGAMOTO
ya usafiri nchini, hususan maeneo ya vijijini kuwa historia baada ya
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa kuzindua Wakala wa Barabara za Vijijini na
Mijini (TARURA).
Amesema
wakala huo utasaidia kuimarisha mtandao wa barabara za vijijini na
kuwawezesha wananchi wengi kusafiri na kusafirisha bidhaa zao kwa
urahisi, hivyo kukuza uchumi.
Waziri
Mkuu ameyasema hayo leo (Jumapili, Julai 02, 2017) wakati akizindua
wakala huo katika ukumbi wa Chuo cha Mipango, mjini Dodoma.
“Wakala
huu tunaouzindua leo utakuwa na manufaa makubwa kwa ustawi wa nchi yetu
kwa kuongeza chachu ya uzalishaji mali mashambani kutokana na urahisi
wa kufika sokoni,”
“Utashusha
bei ya vyakula mijini na bidhaa za viwandani vijijini kutokana na
gharama za usafirishaji wa mazao kutoka mashambani na bidhaa za
viwandani kutoka mijini kupungua,”
Aidha,
Waziri Mkuu amesema manufaa mengine ya wakala huo ni kuboresha na
kubadili hali za kimaisha na kiuchumi kwa wananchi kwani watakuwa
wanasafiri kwa muda mfupi.
Pia utawezesha maeneo mengi ya nchi kufikika kwa urahisi, hivyo kuboresha utoaji wa huduma za kijamii kwa wakati.
Katika hatua nyingine,
Waziri Mkuu amesema Mamlaka za Serikali za Mitaa zinakabiliwa na
changamoto mbalimbali katika ujenzi, ukarabati na utengenezaji wa
miundombinu ya barabara ikiwemo ya rushwa katika utoaji wa zabuni.
Amesema
jambo hilo halikubaliki hivyo, amewataka watendaji wa TARURA
wahakikishe wanatokomeza vitendo vya rushwa vilivyokithiri kwenye utoaji
wa zabuni, zitolewe kwa watu wenye uwezo wa kufanyakazi.
Waziri
Mkuu amesema changamoto nyingine ni usimamizi hafifu wa mikataba ya
ujenzi, ambapo ameelekeza isimamiwe vizuri na iwe ya wazi na yenye
kutekelezeka.
Akizungumzia
vitendo vya baadhi ya viongozi wa Halmashauri kubadilisha matumizi
fedha za barabara, ameagiza fedha zote zinazotengwa kwa ajili ya miradi
ya barabara zitumike kama ilivyopangwa.
Awali,
Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais-TAMISEMI, Mheshimiwa George Simbachawene
alisema TARURA ni muhimu kwa kuwa zinagusa wananchi moja kwa moja na ni
kichocheo kikubwa cha uchumi wa wananchi, hivyo kuinua uchumi wa Taifa
wenye msingi imara.
“Barabara
hizi zinachochea kilimo katika ngazi ya jamii, zinaboresha ufikaji
kwenye huduma za kijamii kama afya, elimu, maji na masoko, hivyo
kuliwezesha Taifa kuwa na jamii imara kiafya, kiakili na kiuchumi,”.
Kutokana
na umuhimu wa mtandao wa barabara za Vijijini na Mijini, Mheshimiwa
Simbachawene ameomba mgawanyo wa mapato ya Mfuko wa Barabara wa asilimia
70 kwa TANROADS na asilimia 30 kwa Halmashauri uangaliwe upya, ambapo
Waziri Mkuu ameridhia.
Waziri
Mkuu alisema “Naamini kwa kuanzishwa TARURA sasa hoja hii inajadilika,
tumieni taratibu zilizopo ili maamuzi yaweze kufanyika,”.
Mtandao wa barabara za Mamlaka ya Serikali za Mitaa ni kilomita 108,942.2 ambao ni Zaidi ya nusu ya barabara za Kitaifa.
EmoticonEmoticon
Note: Only a member of this blog may post a comment.