Thursday, July 27, 2017

UKATILI DHIDI YA WANAWAKE NA WATOTO WAJADILIWA.


Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera na Uratibu) Dkt. Hamisi Mwinyimvua ameongoza kikao cha Makatibu Wakuu cha Kujadili na kuupitisha Mwongozo wa Uratibu wa Mpango Kazi wa Taifa wa Kutokomeza Ukatili Dhidi ya Wanawake na Watoto nchini.

Kikao hicho kilichofanyika Ofisi ya Waziri Mkuu Dodoma Julai 27, 2017 ambapo kilihusisha Makatibu wakuu pamoja na wadau wa maendeleo kwa lengo la kujadili mwongozo huo ili kuhakikisha utekelezaji wake unaanza mapema iwezekanavyo.

Akizungumza wakati wa kikao hicho Dkt. Mwinyimvua alieleza umuhimu wa mwongozo ikiwa ni nyenzo muhimu ya kusaidia kutatua changamoto zinazowakabili wanawake na watoto ambapo kabla ya kuandaliwa Mwongozo huo, Tanzania ilikuwa na mipango kazi minane (8) ya kuzuia ukatili dhidi ya wanawake na watoto.

“Lengo la Mwongozo huu ni kupunguza masuala ya ukatili kwa watoto na wanawake hivyo ni vyema ukajadiliwa na kuanza utekelezaji wake mapema ili kutatua changamoto za wanawake na watoto katika jamii.”Alisema Dkt.Mwinyimvua

Aidha mwongozo huo umeainisha mambo ya msingi yanayohusu masuala ya wanawake na watoto kwa kuangalia sheria mbalimbali zinazowalinda katika maisha yao ya kila siku ili kuwasaidia katika utekelezaji wa majukumu yao kwa kuzingatia haki na usawa.

Kwa upande wake Katibu Mkuu Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Bi. Sihaba Nkingaamesema kuwa wanawake na watoto ndiyo wahanga wakubwa wa vitendo ya ukatili katika jamii hivyo Mwongozo huu ni nyenzo itakayoleta ufanisi katika kutatua vitendo vya ukatili dhidi yao na kuhakikisha haki na usawa vinakuwepo ndani ya jamii.

Mwongozo wa Uratibu wa Mpango Kazi wa Taifa wa Kutokomeza Ukatili Dhidi ya Wanawake na Watoto nchini utaleta ufanisi na kusaidia masuala ya ukatili wa wanawake na watoto hapa nchini hivyo ni vyema kila mdau alione hili na kuunga mkono jitihada za Serikali katika kupambana na vita hii”.alisema Bi.Sihaba

Juhudi hizi zinafanyika ikiwa ni moja ya maadhimio ya nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa, wakuu wa nchi wanachama ambapo kwa pamoja waliadhimia kutokomeza ukatili huo kupitia utekelezaji wa lengo Na. 5 na 6 ya Malengo ya Maendeleo Endelevu ifikapo 2030.

“Uwepo wa mwongozo huu utasaidia kupunguza athari za matokeo ya ukatili dhidi ya wanawake na watoto angalau kwa asilimia 50 ili kundi hili liendelee kuchangia katika maendeleo ya nchi yetu”.Alisisitiza Bi.Sihaba

Naye Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Dkt. Zainabu Chaula alipongeza hatua zilizofikiwa na kuona kuwa ni mpango mzuri utakao fikia malengo yaliyokusudiwa ya kupunguza vitendo vya ukatili dhidi ya wanawake na watoto nchini.

“Niipongeze Serikali kwa kuendelea na jitihada hizi ikiwemo kuwepo kwa mwongozo huu ambapo utatupa dira ya kuyafikia malengo yaliyokusudiwa juu mapambano ya vitendo vya ukatili kwa wanawake na watoto”.Alieleza Dkt. Zainabu.

AWALI:Mwongozo huo ulizinduliwa rasmi tarehe 13 Desemba, 2016 na Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee  na Watoto Ummy Mwalimu kwa niaba ya Makamu wa Rais Samia Suluhu Hassan Jijini Dar es Salaam.


EmoticonEmoticon

Note: Only a member of this blog may post a comment.