WAZIRI MKUU
Kassim Majaliwa amefanya ziara katika hospitali ya wilaya ya Ruangwa na amekabidhi
magari mawili ya kubebea wagonjwa.
Amesema kati
ya magari hayo moja ni kwa ajili ya hospitali hiyo ya wilaya na la pili litapelekwa
katika kituo cha afya cha Mandawa.
Waziri
Mkuu amekabidhi magari hayo leo (Jumatano, Julai 12, 2017), alipotembelea
hospitali hiyo, ikiwa ni siku ya tatu ya ziara yake ya kikazi Mkoani Lindi.
Amesema magari hayo ni muendelezo wa mkakati wa Serikali
ya awamu ya tano wa kuboresha huduma za afya kwa wananchi wake.
“Rais wetu Dkt.
John Magufuli amedhamiria kuwaondolea wananchi kero mbalimbali zinazowakabili zikiwemo
za huduma za afya, hivyo tuendelee kumuunga mkono.”
Waziri Mkuu amesema magari hayo ya kisasa yatasaidia kurahisisha
usafiri kwa wagonjwa wanaohitaji
matibabu ya dharura katika hospitali kubwa.
Kabla ya kukabidhi magari hayo, Waziri Mkuu
alitembelea wodi ya akina mama na ya watoto waliolazwa katika hospitali hiyo na
amesema kwamba ameridhishwa na hali ya utoaji huduma.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Halmashauri ya wilaya
ya Ruangwa, Mheshimiwa Rashid Nakumbya amesema magari hayo ni faraja kwao kwa
kuwa walikuwa na changamoto ya usafiri kwa wagonjwa wa dharura.
“Tunatambua
na kuthamini jitihada kubwa zinazofanywa na Serikali ya awamu ya tano katika
halmashauri yetu na Taifa kwa ujumla, nasi tutayatumia magari haya kama
ilivyokusudiwa.”
Awali, Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya
Wilaya ya Ruangwa, Dkt. Regan Rajuu amesema hali ya upatikanaji wa dawa na
vifaa tiba katika hospitali hiyo umeongezeka kutoka asilimia 80 Desemba, 2016
na kufikia asilimia 90 Juni 2017.
Pia Waziri Mkuu
alitembelea shule ya Sekondari ya Kassim Majaliwa iliyoanza kujengwa Desemba,
23, 2016 kwa michango ya Halmashauri, fedha za mfuko wa jimbo pamoja na wadau
mbalimbali wa maendeleo.
Kaimu Mkuu wa
shule hiyo, Mwalimu Emmanuel Sechawe alisema msingi wa kuanzisha shule hiyo
ulitokana na uwepo wa wanafunzi 319 waliofaulu darasa la saba mwaka 2016 kukosa
nafasi ya kujiunga na kidato cha kwanza katika shule zilizopo.
Mbali na
kutembelea shule hiyo, pia Waziri Mkuu alifanya ukaguzi wa maendeleo ya mradi
wa ujenzi wa gereza la wilaya ya Ruangwa, ambalo litakapokamilika litapunguza
msongamano wa wafungwa na mahabusu katika gereza la wilaya ya Nachingwea.
EmoticonEmoticon
Note: Only a member of this blog may post a comment.