Monday, July 31, 2017

WAZIRI MKUU AWAKABIDHI KAPUNGA NA WENZAKE 11 KWA KAMANDA WA TAKUKURU

*Ni baada ya kulisababishia Jiji la Mbeya hasara ya sh. bilioni 63

WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa amemuagiza Kamanda wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) mkoa wa Mbeya Bw. Emanuel Kiabo kumkamata na kumuhoji Mheshimiwa Atanas Kapunga aliyekuwa Meya wa Jiji la Mbeya na wenzake 11 kwa tuhuma za kuisababishia Serikali hasara ya sh. bilioni 63.448.

"Serikali hii haiwezi ikawaacha watu hawa ambao wameisababishia hasara kubwa kiasi hiki tena kwa halmashauri moja. Kama wako humu ndani nagiza wakamatwe na waanze kuhojiwa na ambao wamestaafu au kuhamishwa kituo cha kazi wasakwe popote walipo ili nao waje kuhojiwa.”

Waziri Mkuu ametoa agizo hilo leo (Jumatatu, Julai 31, 2017) alipozungumza na watumishi wa Halmashauri za wilaya ya Mbeya na Halmashauri ya Jiji la Mbeya katika mkutano uliofanyika ukumbi wa Benjamin Mkapa.

Wengine ni waliowahi kuwa wakurugenzi wa Jiji hilo ambao ni Bw. Mussa Zungiza, Bi. Elizabeth Munuo, Bw. Juma Idd na Dkt. Samwel Lazaro aliyekuwa akikaimu nafasi ya Ukurugenzi.

Aliyekuwa Mweka Hazina wa Jiji, Bw. James Jorojik pamoja na waliokuwa wajumbe wa Bodi ya Zabuni ambao ni Bw. Mussa Mapunda, Bw. Samweli Bubengwa, Bw. Davis Mbembela, Bi. Lydia Herbert na Bw. Bernard Nsolo ambao walipitisha nyongeza ya mradi huo bila ya kuzingatia maslahi ya Jiji pamoja Emily Maganga ambaye hakuishauri vizuri bodi hiyo.

Waziri Mkuu amesema watumishi hao wanatakiwa kuchukuliwa  hatua stahiki za kisheria kwa kuwa wameisbabishia Serikali harasa kubwa katika mradi wa ujenzi wa soko la Mwanjelwa Jijini Mbeya ambalo hadi sasa  halijaonyesha tija.

Amesema mradi huo wa soko la Mwanjelwa uligubikwa na changamoto nyingi kuanzia hatua za awali ambapo hata uchukuaji wa mkopo haukuwa umezingatia mpango mkakati wa biashara, hivyo kusababisha Halmashauri ya Jiji kuchukua mkopo zaidi ya kiasi kilichokusudiwa.

Waziri Mkuu amesema mbali na kuzidisha kiasi cha mkopo pia baada ya kukamilika kwa ujenzi watuhumiwa hao waligushi mikataba ya upangaji, jambo ambalo ni kinyume na  matakwa ya Sheria ya Manunuzi ya Umma. Pia waligawa vizimba kwa wafanyabiashara bila ya kupitia mchakato wa manunuzi.

Amesema hata wahanga ambao walikuwepo awali kabla ya kuungua kwa soko hawakupewa kipaumbele katika mchakato wa upangishaji wa soko jipya, ambapo kwa hali ya kawaida ilitarajiwa wangekuwa wa kwanza kufikiriwa kutokana na hasara waliyoipata baada ya kuunguliwa mali zao.

Pia Waziri Mkuu amemuagiza Mkuu wa Mkoa wa Mbeya. Bw. Amos Makalla kukutana na Madiwani wa Halmashauri ya Jiji na kuweka mikakati na namna gani wataweza kupanga bei ya vizimba katika soko hilo ili wafanyabiashara wapange na wao kuweze kuanza kupata fedha za kupunguza deni.


EmoticonEmoticon

Note: Only a member of this blog may post a comment.