Friday, July 21, 2017

WAZIRI MKUU AAGIZA UJENZI WA HOSPITALI TUNDUMA

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa ameuagiza uongozi wa Halmashauri ya Mji wa Tunduma wilayani Momba kuanzisha mradi wa ujenzi wa hospitali.

Amesema sh. milioni 900 zilizotengwa kwa ajili ya ujenzi wa ofisi ya Halmashauri kwa sasa zianze kutumika katika kuanzisha ujenzi wa hospitali hiyo.

Agizo hilo alilitoa jana jioni (Ijumaa, Julai 21, 2017) wakati akizungumza na wananchi katika mkutano wa hadhara uliofanyika uwanja wa Shule ya Msingi Tunduma.

“Kwa kuwa afya ni jambo muhimu katika utekelezaji wa kauli mbiu ya Rais Dkt. John Magufuli ya Hapa Kazi Tu, hivyo naagiza fedha zilizotengwa kuanza ujenzi wa ofisi zitumike katika ujenzi wa hospitali.”

Waziri Mkuu aliwataka viongozi wa halmashauri hiyo kuongezea sh. milioni 126 katika ujenzi huo. Fedha hizo zilitengwa  kwa ajili ya kuwafidia wamiliki wa eneo lililotengwa awali kwa ajili ya kujenga hospitali, ambapo aliwataka watafute eneo lisilohitaji fidia.

Pia, Waziri Mkuu aliuagiza uongozi wa Wakala wa Majengo Tanzania (TBA) iandae ramani kwa ajili ya ujenzi wa hospitali hiyo na kuhusu suala la ujenzi wa ofisi Serikali italishughulikia.

Waziri Mkuu alitoa agizo hilo baada ya Mbunge wa jimbo la Tunduma, Mheshimiwa Frank Mwakajoka aliyeiomba kuiomba Serikali kuwajengea hospitali kwa kuwa halmashauri hiyo haina hospitali, hivyo kusababisha usumbufu mkubwa kwa wananchi pale wanapohitaji huduma hiyo.

Naye Mkuu wa wilaya hiyo, Bw. Juma Irando alitaja baadhi ya changamoto zinazoikabili wilaya hiyo kuwa ni ukosefu wa hospitali ya wilaya, ukosefu wa ofisi ya Mkuu wa Wilaya na ofisi za Halmashauri.

Pia changamoto nyingine ni ubovu wa miundombinu ya barabara iliwemo ya Makamba-Ikana inayotakiwa kukarabatiwa inayounganisha ukanda wa juu na chini ili wananchi wa ukanda wa juu waweze kufika makao makuu ya wilaya.



EmoticonEmoticon

Note: Only a member of this blog may post a comment.