WAZIRI MKUU Kassim
Majaliwa amesema kuanzia mwaka huu wa fedha, Serikali imepunguza gharama za malipo ya awali ya thamani ya
ardhi iliyopimwa kutoka asilimia 7.5 hadi asilimia 2.5.
“Serikali inaendelea kupunguza gharama za umilikaji wa ardhi
nchini na katika mwaka
wa fedha 2017/2018, imepunguza tozo ya awali ya
ardhi iliyopimwa (premium) kutoka asilimia 7.5 ya thamani ya ardhi hadi asilimia 2.5 tu.
Natoa wito kwa wananchi kuchangamkia punguzo hili na kujitokeza kupimiwa na
kumilikishwa ardhi,” amesisitiza.
Waziri Mkuu
ametoa kauli hiyo leo (Jumatano, Julai 5, 2017), bungeni mjini Dodoma wakati akitoa hoja ya kuahirisha mkutano wa saba wa
Bunge la 11. Bunge limeahirishwa hadi Septemba 5, mwaka huu.
Amesema Serikali
itahakikisha kuwa kila kipande cha ardhi ya Tanzania kinapimwa ikiwa ni
utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2015. “Serikali imeweka mkakati na mpango kazi wa kuwezesha kufikia lengo la
kupanga matumizi bora ya
ardhi katika vijiji 1,500 na wilaya tano kila mwaka.”
Amesema Serikali itaendelea kuimarisha Ofisi za Ardhi za
Kanda kwa kupeleka wataalam wa kada mbalimbali na kuwawezesha kwa kuwapatia
vitendea kazi stahiki. “Kazi ya upimaji wa ardhi haiwezi
kufanikiwa bila ya rasilmali watu. Lengo letu ni kuwawezesha
wananchi kupata huduma mbalimbali za ardhi katika kanda badala ya kufuata
huduma hizo makao makuu ya wizara,” amesema.
Amewasihi watumishi watakaohamishiwa katika ofisi za kanda pamoja na wale waliopo katika
Halmashauri, wafanye kazi kwa ushirikiano na watekeleze majukumu yao kwa
kuzingatia sheria, kanuni na taratibu
zinazosimamia sekta ya ardhi na kutoa huduma kwa wananchi bila ubaguzi wa aina
yoyote.
EmoticonEmoticon
Note: Only a member of this blog may post a comment.