Saturday, July 29, 2017

WAZIRI MKUU ATOA SIKU MBILI KWA MADIWANI KYELA KUMALIZA TOFAUTI ZAO

*Amesema wakiendelea Serikali itavunja Baraza

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amewapa siku mbili Madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Kyela Mkoani Mbeya kumaliza tofauti zao zinazokwamisha utendaji wa Halmashauri hiyo na kuendelea kufanya kazi walizotumwa na wananchi.

Tofauti hizo ambazo zimedumu kwa takriban mwaka mmoja zmesababisha Madiwani hao kushindwa kufanya vikao jambo linalokwamisha shughuli za maendeleo ya wananchi katika Halmashauri hiyo.

Waziri Mkuu ametoa agizo hilo leo (Jumamosi, Julai 29, 2017) wakati akizungumza na watumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kyela akiwa katika ziara yake ya kikazi Mkoani Mbeya.

Amesema ikifika Jumatatu (Julai, 31, 2017) Madiwani hao wawe wamemaliza tofauti zao na wawaite wakuu wa Idara na kuwapa taarifa hiyo ili shughuli za maendeleo ziendelee kutekelezwa ndani ya Halmashauri hiyo.

"Baraza la Madiwani limegawanyika mnamgogoro tunataka uishe na mshirikiane na mshikamane katika kufanya shughuli za maendeleo ili wananchi waweze kupata manufaa. Mkiendeleza migongano hatutawavumilia Serikali inauwezo wa tutalivunja baraza."

Amesema baadhi ya Madiwani hao wanawatetea watumishi waliosimamishwa kazi kwa tuhuma za kuiibia Serikali mabilioni ya fedha jambo ambalo halikubaliki na halivumiliki. “Naombeni mmalize tofauti zenu mara moja kabla sijaondoka.”

Hata hivyo, Waziri Mkuu ameiagiza Taasisi ya Kupambana na Kuzuia Rushwa (TAKUKURU) mkoa wa Mbeya kuhakikisha watumishi wote waliohusika katika kula fedha za umma wanachukuliwa hatua kama alivyopendekeza Mkaguzi na Mdhibiti wa Hesabu za Serikali(CAG).

Pia aliwahasa watumishi wa umma kuhakikisha wanatimiza wajibu na majukumu yao kikamilifu kwa kufanya kazi kwa bidi na kuacha ubabaishaji na kufanya kazi kwa mazoea na badala yake wawahudumie wananchi ipasavyo.


EmoticonEmoticon

Note: Only a member of this blog may post a comment.