*Asema Serikali yatenga sh. bilioni 412 kwa miradi ya maendeleo
WAZIRI MKUU
Kassim Majaliwa amesema Serikali haina mpango wa kuanzisha maeneo mapya ya
utawala hadi ikamilishe kuboresha miundombinu kwenye maeneo iliyoyaanzisha.
“Ili
kutimiza azma hiyo, Serikali katika mwaka wa fedha 2017/2018 imetenga kiasi cha shilingi bilioni 412.38 kwa ajili ya miradi ya maendeleo. Kati ya fedha
hizo, Serikali imetenga shilingi bilioni 16.985 kwa ajili ya kuboresha miundombinu
ya majengo ya ofisi na makazi ya viongozi katika mikoa yote mipya,” amesema Waziri Mkuu.
Waziri Mkuu
ametoa kauli hiyo leo (Jumatano, Julai 5, 2017), bungeni mjini Dodoma wakati akitoa hoja ya kuahirisha mkutano wa saba wa
Bunge la 11. Bunge limeahirishwa hadi Septemba 5, mwaka huu.
“Katika
mgawo huo, mkoa wa Njombe umetengewa jumla ya shilingi bilioni 3.34; mkoa wa
Katavi umetengewa jumla ya shilingi bilioni 3.080; mkoa wa Simiyu umetengewa
jumla ya shilingi bilioni 3.775, mkoa wa Geita umetengewa jumla ya shilingi
bilioni 2.978 na mkoa wa Songwe umetengewa jumla shilingi bilioni 3.812,”
amesema.
Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu amesema Serikali
imetenga jumla ya shilingi bilioni 61.7 kwa ajili ya ujenzi wa makao makuu ya
Halmashauri 64 ambapo kati ya fedha hizo, shilingi bilioni 28.7 ni kwa ajili ya
kukamilisha majengo ya ofisi katika Halmashauri 44 na shilingi bilioni 33 ni
kwa ajili ya ujenzi wa makao makuu ya Halmashauri mpya 20.
Sambamba na hatua
hizo, Serikali kupitia Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Wazee na Watoto
imetoa vifaa mbalimbali kwa ajili ya kuboresha huduma za afya katika Mamlaka za
Serikali za Mitaa vyenye thamani ya shilingi bilioni 2.9 pamoja na kununua magari ya kubebea wagonjwa katika Halmashauri 67.
Waziri
Mkuu amesema miongoni mwa hatua
zinazochukuliwa na Serikali ni pamoja na kuendeleza juhudi za ugatuaji wa
madaraka kwenda katika Mamlaka za Serikali za Mitaa pamoja na kuongeza mgawo wa
fedha za ruzuku ya maendeleo inayopelekwa kwenye
vyombo hivyo.
Amesema Serikali
inachukua hatua hizo ili kuhakikisha kuwa Mamlaka za Serikali za Mitaa nchini
zinatimiza malengo ya kuanzishwa kwake kwa mujibu wa Ibara ya 145 na 146 ya
Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, 1977.
EmoticonEmoticon
Note: Only a member of this blog may post a comment.