Monday, July 24, 2017

WAZIRI MKUU AELEKEZA NAMNA YA KUMALIZA MGOGORO ARDHI KATI YA WANANCHI NA KIWANDA CHA SARUJI MBEYA

WAZIRI Mkuu Kassim Majaliwa, ametoa maelekezo ya namna ya kumaliza mgogoro wa ardhi uliodumu kwa zaidi ya miaka sita, kati ya uongozi wa Kiwanda cha Saruji Mbeya na wananchi wa kijiji cha Nanyala, wilayani Mbozi.

Mgogoro huo, umetokana na Kiwanda cha Saruji Mbeya, kupewa  eneo la kijiji hicho chenye ekari 2,315 na uongozi wa mkoa wa Mbeya bila ya makubaliano na wanakijiji hali iliyosababisha wagome kuondoka.

Pia Waziri Mkuu amewaagiza wakuu wa Mikoa ya Songwe Luteni Mstaafu Chiku Gallawa  na wa Mbeya Bw. amos Makalla kukutana na kufanya mazungumzo ya kulirudisha eneo hilo mkoa wa Songwe.

Waziri Mkuu alitoa uamuzi huo leo (Jumatatu, Julai 24, 2017) baada ya wananchi wa kijiji hicho kuzuia msafara wake kwa lengo la kumuelezea changamoto yao ya kudhulumiwa ardhi yao na kukabidhiwa kwa muwekezaji bila ya kushirikishwa.

Amesema Serikali ya awamu ya tano chini ya Mheshimiwa Rais Dkt. John Magufuli ni sikivu na inawajali wanyonge ndio maana amesimama ili aweze kusikiliza kero zao na kuzipatia ufumbuzi, hivyo amewaomba  waendelee kuiamini na watarudishiwa ardhi yao.

Pia, Waziri Mkuu ameiagiza Kampuni ya Saruji Mbeya kuondoa kesi iliyoifungua mahakamani dhidi ya wananchi wa eneo hilo, ili waweze kukutana na Serikali pamoja na wananchi hao kwa ajili ya kujadili namna bora ya uwekezaji katika eneo hill.

Amesema kiwanda hicho kilipewa eneo hilo la mkoa wa Songwe kimakosa na mkoa wa Mbeya kwa ajili ya kupata malighafi ya kutengenezea saruji, amesema Serikali haiwazuii kulitumia eneo hilo ila wakubaliane na wananchi kwanza.

“Hatuzuii kiwanda kufanya kazi ila tunataka mkubaliane na wananchi kwanza ili kuondoa migogoro. Wananchi wanahitaji viwanda ila si kwa migogoro. Wananchi nawaomba muendelee kuwa na amani na hakuna atakayechukua ardhi yao bila ya ridhaa yao.”

Eneo hilo lilikuwa mali ya Serikali toka mwaka 1987, ambapo wakati Kampuni ya Saruji Mbeya ilikuwa inamilikiwa na Serikali, kabla ya kubinafsishwa.

Wananchi hao wamesema wamefurahishwa na uamuzi huo wa Waziri Mkuu wa kutatua mgogoro huo ambapo wananchi hao walidai kwa muda mrefu ulikuwa ukiwasumbua kwa kutakiwa kuondoka katika eneo lao bila na kukabidhiwa kwa muwekezaji bila ya kushirikishwa.

Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Songwe amemshukuru Waziri Mkuu kwa kulitolea tamkoa suala hilo na kwamba atakutaka na Mkuu wa Mkoa wa Mbeya kwa ajili ya utekelezaji wa agizo hili ili wananchi waweze kuishi kwa amani katika ardhi yao.


EmoticonEmoticon

Note: Only a member of this blog may post a comment.