Tuesday, July 11, 2017

WAZIRI MKUU ATEMBELEA UJENZI WA DARAJA MTO LUKULEDI

*Asema watu wengi wamekufa wakikatiza katika eneo hilo

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa ametembelea mradi wa ujenzi wa daraja la mto Lukuledi lenye urefu wa kilomita 30.45 linalounganisha mikoa ya Lindi na Mtwara na na  kusema kwamba ameridhishwa na maendeleo ya ujenzi wake.

Amesema ujenzi wa daraja hilo unatakaogharimu sh. bilioni 5.4 ni mkombozi kwa wananchi wa mikoa hiyo hasa wa wilaya za Ruangwa na Masasi ambao kwa muda mrefu wamekuwa wakishirikiana  katika masuala mbalimbali yakiwemo kilimo na huduma za kijamii.

Waziri Mkuu amesema hayo leo (Jumanne, Julai 11, 2017) alipotembelea mradi huo wa ujenzi wa daraja hilo katika kijiji cha Nandanga alipowasili wilayani Ruangwa akiwa katika siku ya pili ya ziara yake ya kikazi ya siku nne Mkoani Lindi.

“Watu wengi wamepoteza maisha kwa kuliwa na mamba walipokuwa wakikatiza katika eneo hilo. Ujenzi wa daraja hili ni muhimu, watu wengi wa Ruangwa wanavuka kufuata matibabu katika hospitali ya Ndanda, wilayani Masasi na wakazi wa Ndanda wanavuka kufanya shughuli za kilimo wilayani Ruangwa.”

Pia Waziri Mkuu amewaomba wananchi wa maeneo hayo kuhakikisha wanatoa ushirikiano kwa mkandarasi anayejenga daraja hilo ili aweze kutekeleza majukumu yake ipasavyo na kumaliza mradi huo kwa wakati.

Kwa upande wake Mbunge wa jimbo la Ndanda, Mheshimiwa Cecil Mwambe ameipongeza na kuishukuru Serikali kwa jitihada zake za kuwaletea wananchi maendele0 na kubadilisha maisha yao.

Amesema mradi wa ujenzi wa daraja hilo ni faraja kwa wananchi wa mikoa hiyo kwa kuwa eneo hilo ni makazi ya mamba, hivyo kukamilika kwake kutaokoa maisha ya watu pamoja na kurahisisha usafiri wa watu na bidhaa.

Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu amesema changamoto ya upatikanaji wa huduma ya maji safi na salama katika vijiji vya Litama, Luchelegwa, Nandanga, Ipingo na Chiapi kuwa historia baada kuungwanishwa na mradi wa maji wa Mbwinji.

Ameyasema hayo leo wakati akizungumza kwa nyakati tofauti na wananchi wa vijiji vya Litama, Chiapi, Nandanga, Luchelegwa alipowasili wilayani Ruangwa akiwa katika siku ya pili ya ziara yake ya kikazi ya siku nne Mkoani Lindi.

Waziri Mkuu amesema Serikali inatekeleza  Kampeni yake ya  kumtua mama ndoo, hivyo itahakikisha wananchi katika maeneo yote nchini, hususan ni ya vijijini wanapata huduma ya maji safi na salama katika umbali usiozidi mita 400.

Ameitoa kauli hiyo baada ya wananchi wa vijiji hivyo kumueleza changamoto mbalimbali zinazowakabili kwenye maeneo yao zikiwemo za maji, barabara, umeme, ambapo aliwahakikishia kwamba Serikali imeshaanza kuboresha huduma hizo.


Wakati huo huo, Waziri Mkuu amezindua Zahanati  ya Nandanga ambayo imejengwa kwa fedha kutoka mfuko wa jimbo umegaharimu kiasi cha sh. milioni 73.47 na kuwahakikishia kwamba  Serikali itawapelekea  wataalam wa kutosha ili kuwahudumia.


EmoticonEmoticon

Note: Only a member of this blog may post a comment.