Thursday, February 14, 2019

WAZIRI MKUU: NBC ONGEZENI WIGO WA BIASHARA

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa ameitaka Benki ya Biashara nchini (NBC) iongeze wigo wake ili iweze kutoa huduma kwa wananchi wengi zaidi.

Ametoa wito huo leo (Alhamisi, Februari 14, 2019)  wakati akizungumza na Mkurugenzi Mtendaji wa benki hiyo, Bw. Theobald Sabi ofisini kwake Magogoni, jijini Dar es Salaam.

“Ninatoa wito kwenu mpanue wigo katika utoaji wa huduma zake hapa nchini ili kuwawezesha wananchi wengi zaidi kuhifadhi fedha zao katika eneo salama,” amesema Waziri Mkuu.

Amesema wakati Serikali ikiendelea kuhamasisha wananchi waongeze nguvu katika sekta ya kilimo, taasisi za fedha hazina budi kusogeza huduma zao karibu na wananchi ili waweze kutunza fedha zao katika hali ya usalama badala ya kuzihifadhi majumbani.

Waziri Mkuu ametumia fursa hiyo kuipongeza benki  ya NBC kwa kuunga mkono juhudi za Serikali za kuwawezesha wananchi kupitia mikopo kwa wajisiriamali wadogo ambayo inawawezesha kuongeza mitaji yao ya biashara mbalimbali.

Kwa upande wake, Mkurugenzi huyo wa NBC amesema ameishukuru Serikali kwa kuwatengenezea mazingira mazuri ya kufanya biashara na mwaka wa fedha uliopita wamefanikiwa kutengeneza faida na kwamba wanatarajia kutoa tena gawio. Hata hivyo, hakutaja ni kiasi gani cha gawio kitatolewa, kwa sababu anasubiri uamuzi wa Bodi.
 
Pia amemkabidhi Waziri Mkuu hundi yenye thamani ya shilingi 11,270,000 ambazo amesema zitasaidia katika ujenzi wa kituo cha polisi wilayani Ruangwa.

(mwisho)


EmoticonEmoticon

Note: Only a member of this blog may post a comment.