Thursday, February 7, 2019

ZAIDI YA SH. BIL. 500 ZIMELIPWA KWA WAKULIMA WA KOROSHO-MAJALIWA

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema zaidi ya sh. bilioni 500 zimelipwa kwa wakulima wa korosho kati ya sh. bilioni 700 zinazotarajiwa na kwamba malipo hayo bado yanaendelea kulipwa kwa wakulima wengine waliosalia.

Amesema tamko la Rais Dkt. John Magufuli la kwamba Serikali itanunua korosho kwa bei ya sh. 3,300 ni kwa ajili ya korosho za daraja la kwanza  na bei ya korosho za daraja la pili ni asilimia 80 ya zile za daraja la kwanza.

Ametoa kauli hiyo leo asubuhi (Alhamisi, Februari 7, 2019) Bungeni jijini Dodoma katika kipindi cha maswali ya papo kwa papo kwa Waziri Mkuu wakati akijibu swali la Mbunge wa Liwale, Zuberi Kuchauka.

Mbunge huyo alitaka kupata kauli ya Serikali kuhusu malipo kwa wakulima wa korosho ambao walikuwa wakilipwa sh. 2,600 kwa kilo wakati Rais Dkt.  Magufuli alisema Serikali itanunua kilo moja ya korosho kwa sh. 3,300.

“Malipo yanaendelea na sehemu kubwa ni kwa wakulima wenye kilo zaidi ya 1,500, Serikali itanunua korosho zote kama ilivyoelezwa. Taratibu zinazofanyika ni kuhakikisha anayelipwa ni muhusika. Wananchi endeleeni kuiamini Serikali yenu.”

Waziri Mkuu amesema ilikuwa ni lazima kwa Serikali ifanye uhakiki kwa wakulima hususani wale wenye kilo zaidi ya 1,500 ili kujiridhisha kama ni wakulima, hivyo baada ya kuhakikiwa wakulima wote watalipwa fedha zao.

Amesema Januari 27, 2019 alitoa maagizo kwa Wizara ya Kilimo pamoja na Bodi ya Mazao Mchanganyiko wahakikishe hadi Februari 15 mwaka huu wawe wamekamilisha zoezi la uhakiki na kuwalipa wakulima wote wa zao la korosho.

Waziri Mkuu alitoa agizo hilo wakati akizungumza na wadau wa zao la korosho kwenye kikao kilichofanyika mkoani Mtwara, lengo la kikao hicho ilikuwa ni kupata taarifa juu ya mwenendo mzima wa bidhaa hiyo kwa msimu wa mwaka 2018/2019.

Wakati huo huo, Waziri Mkuu amesema Serikali haijakiuka sheria kuhusu suala la watumishi kupandishwa mishahara na kwamba ina nia njema ya kuhakikisha wanalipwa mishahara na posho nzuri.

Ameyasema hayo wakati akijibu swali la Mbunge wa Mbozi, Pascal Haonga aliyedai Serikali imekiuka sheria ya utumishi kwa kutopandisha mishahara, ambapo Waziri Mkuu amesema  Serikali haikukiuka sheria, bali iliamua kushughulikia suala hilo kwa kuanza na uhakiki wa watumishi.

Waziri Mkuu amesema baada ya kufanya uhakiki na kubaini uwepo kwa watumishi hewa pamoja na waliokuwa wakitumia vyeti vya kugushi, iliwaondoa na sasa Bodi ya Mishahara na Maslahi ya Watumishi wa Umma inafanya mapitio ya mishahara baada ya kubaini tofauti, hivyo watumishi waendelee kuwa watulivu.


(mwisho)


EmoticonEmoticon

Note: Only a member of this blog may post a comment.