Friday, February 15, 2019

WAZIRI MKUU AKARIBISHA WAWEKEZAJI NCHINI

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akisalimiana na Balozi wa Falme za Kiarabu Nchini Ibrahim Abdullah, wakati akimkaribisha kwa mazungumzo, ofisini kwake Magogoni Februari 15, 2019.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza na Balozi wa India Nchini Sandeep Arya, ofisini kwake Magogoni Februari 15, 2019.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza na Balozi wa Misri Nchini Ibrahim Abdullah, ofisini kwake Magogoni Februari 15, 2019.
*Awahakikishia ushirikiano wa kutosha kutoka Serikalini

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amewakaribisha wawekezaji kutoka nchi za India, Misri na Falme za Kiarabu waje wawekeze nchini na Serikali itawapa ushirikiano wa kutosha.

Ameyasema hayo leo (Ijumaa, Februari 15, 2019) wakati alipokutana kwa nyakati tofauti na mabalozi wa India, Misri na Falme za Kiarabu wanaowakilisha nchi zao hapa Tanzania.

Mabalozi aliokutana nao ni  Balozi Sandeep Arya (India), Balozi Mohamed Abulwafa (Misri) na Balozi Mohammad Albahri (Kaimu Balozi wa Falme za Kiarabu nchini Tanzania).

Akizungumza na Mabalozi hao Ofisini kwa Waziri Mkuu, Magogoni, Dar es salam, Waziri Mkuu amesema Tanzania ipo tayari kuwapokea wawekezaji kutoka kwenye nchi hizo.

Amesema Serikali imedhamiria kuendeleza sekta ya viwanda nchini ili kukuza uchumi na kufikia wa kati ifikapo 2025, hivyo amewakaribisha wafanyabiashara waje wawekeze.

Amesema Ofisi yake kupitia Waziri mwenye dhamana ya Uwekezaji, Bibi Angela Kairuki iko tayari kuwasikiliza na kuwasaidia wawekezaji wote wanaokusudia kuwekeza nchini.

“Tanzania iko tayari wakati  wote kutoa ushirikiano ili kuhakikisha wawekezaji watakaojitokeza kuwekeza nchini wanafanikiwa ili mataifa yote yaweze kufaidika.”

Kadhalika, Waziri Mkuu amesema Tanzania ina vivutio vingi vya utalii ikiwa ni pamoja na uwepo wa mlima Kilimanjaro, mbunga zenye wanyama wa aina mbalimbali na fukwe nzuri.
Hivyo, ametumia fursa hiyo kuwakaribisha watalii kutoka mataifa mablimbali yakiwemo yaIndia, Misri na Falme za Kiarabu waje nchini na kutembelea vivutio vya utalii vilivyopo.

Kwa upande wao,Mabalozi hao wameishukuru Serikali kwa ushirikiano mzuri uliopo baina ya Tanzania na nchi zao, hivyo wamemuhakikishia Waziri Mkuu kwamba watauendeleza.

Wamesema wapo tayari kushirikiana na Tanzania kuhakikisha mkakati wa Serikali wa kukuza uchumi kutoka wa chini kwenda wa kati kupitia sekta ya viwanda unafanikiwa. 
Pia Mabalozi hao wameahidi kushirikiana na Serikali Tanzania kuhakikisha inaboresha sekta mbalimbali ikiwemo ya utalii ili kuongeza idadi ya watalii wanaotembelea nchini.

(mwisho)


EmoticonEmoticon

Note: Only a member of this blog may post a comment.