Monday, December 5, 2016

SERIKALI KUENDELEA KUTOA USHIRIKIANO KWA UONGOZI MPYA WA TUCTAWaziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge,  Ajira na watu wenye ulemavu), Jenista Mhagama amesema Serikali itaendelea kutoa ushirikiano wa kutosha kwa viongozi wa Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Nchini (TUCTA) ili kuleta tija na ufanisi katika sekta ya kazi..

Waziri Mhagama aliyasema hayo leo Jijini Dar es Salaam tarehe 05 Desemba, 2016, wakati wa mkutano wake na Viongozi hao wa TUCTA waliofika ofisini kwake kwa ajili ya kujitambulisha mara baada ya kumalizika kwa uchaguzi wa shirikisho hilo.

“Tumefarijika sana kwa TUCTA kupata uongozi mpya ambao tuna uhakika wanachama wamezingatia masuala  muhimu katika uchaguzi wao ikiwemo weledi na kutazama dira ya sekta ya wafanyakazi nchini”.

Aidha aliongeza kuwa Viongozi hao wana jukumu kubwa la kuleta tija na maendeleo chanya katika sekta ya kazi nchini na kuhimiza kuwa wafanyakazi ni rasilimali muhimu katika kuleta maendeleo ya nchi.

Kwa mujibu wa Mhagama ameahidi Viongozi hao kufanya kikao kazi mapema iwezekanavyo kwani uchaguzi umekwisha na sasa kilichobaki ni kufanya kazi.

Pia amesisitiza ushirikiano wa kudumu kati ya Serikali, Waajiri na wafanyakazi ambao utasaidia kwa kiasi kikubwa kutatua migogoro iliyopo.

Kwa upande wake Rais wa TUCTA, Tumaini Nyamghokya alimshukuru Waziri Mkuu Kassim Majaliwa kwa kusimamia utu wa mtumishi kwa kuhaidi kuwalinda kutokana na baadhi ya viongozi kutoa lugha zisizosahihi.

Aidha, ameishukuru Serikali kwa kuwa karibu nao kwa muda wote na kuhaidi kuendeleza ushirikiano huo ili kuleta tija katika kazi.EmoticonEmoticon

Note: Only a member of this blog may post a comment.