WAZIRI
MKUU Kassim Majaliwa amemuagiza Mkuu wa Wilaya ya Karatu Bi. Theresia Mahongo
kuhakikisha mashine zote za kupampu maji zilizoko ndani ya mita 500 kutoka
kwenye chanzo cha maji cha Qangded ziwe zimeondolewa ifikapo saa 12.00 jioni ya
leo na atakayekaidi atachukuliwe hatua za kisheria.
Amesema
kitendo cha kuweka mashine za kupampu maji karibu na chanzo hicho na kuvuta
maji kwenda kwenye mashamba yao kinasababisha maji kushindwa kufika katika
mashamba ya wakulima wengine hivyo amewataka wafuate utaratibu uliowekwa na
waendeshaji wa mradi huo.
Waziri
Mkuu ametoa agizo leo (Jumatatu, Desemba 5, 2016) wakati akizungumza na
wananchi kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika katika kijiji cha Jobaji
kata ya Baray wilayani Karatu, ambapo amesema Serikali haitavumilia kuona mtu
mmoja akivuruga mradi huo wa umwagiliaji.
Amesema
ili kuhakikisha mradi huo wa umwagiliaji unakuwa endelevu lazima chanzo cha
maji kilindwe na wananchi wasiruhusiwe kufanya shughuli za kijamii karibu na
chanzo na badala yake wasogee umbali wa mita 500.
"Sitaki
kuona mashine zikipampu maji ndani ya mita 500 kutoka kwenye chanzo na badala
yake wakulima wote wafuate taratibu zilizowekwa . Lazima chanzo kilindwe kwa
sababu maji yakikauka mazao nayo yatakauka, hivyo tutakosa chakula jambo ambalo
hatutaki litokee. Mkuu wa wilaya kesho nenda kafanye ukaguzi katika chanzo
ukikuta mashine kamata," amesema.
Awali,
Waziri Mkuu alizindua mradi wa maji safi na salama wa kijiji cha Jobaj unaotekelezwa
na shirika la World Vision Tanzania uliogharimu sh. milioni 285. Mradi huo
utahudumia vijiji vitatu vya Kata ya Baray ambavyo ni Mbunga Nyekundu, Jobaj na
Dumbechand.
Kwa
upande wake Mkurugenzi wa Miradi wa Wolrld Vision Tanzania, Bw. Revocutus
Kamara amesema mradi huo unatokana na hitaji kubwa la maji katika vijiji hivyo
vitatu na uwepo wa kisima kirefu cha maji kilichochimbwa kwa ufadhili wa Benki
ya Dunia mwaka 2009.
"Mradi
huu wa maji unatekelezwa kwa awamu tatu, awamu ya kwanza ilianza Machi hadi
Novemba 2016, ambapo wakazi 5,272 ikiwa ni pamoja na taasisi nne za
Serikali ambazo ni Zahanati, Magereza, shule ya msingi na sekondari zilizoko katika
kijiji cha Jobaj wananufaika kwa kupata maji safi na salama," amesema.
Amesema
awamu ya pili na ya tatu ya mradi huo itaanza Disemba 2016 na itagharimu zaidi
ya shilingi milioni 200.
Akizungumza
kuhusu mradi wa umwagiliaji Mkurugenzi huyo amesema shirika lao limechangia
kuboresha miundombinu ya umwagiliaji kwa kujenga kilomita 1.716 za mfereji
katika kijiji cha Jobaj (kilomita moja) na Dumbechand (mita 716) ambapo umegharimu
zaidi ya sh. milioni 210 na inalenga kunufaisha zaidi ya wakulima 4,450 wa
vijiji hivyo.
Amesema mifereji hiyo itawezesha wakulima katika vijiji
hivyo kuwa uhakika wa upatikanaji wa maji kwa ajili ya kilimo cha umwagiliaji
kwa mazao ya chakula na biashara hivyo itasaidia kupunguza migogoro ya maji,
kuongeza eneo la kilimo cha umwagiliaji kutoka hekta 803 hadi hekta 1,203.
EmoticonEmoticon
Note: Only a member of this blog may post a comment.