Sunday, December 4, 2016

WAZIRI MKUU AMALIZA MGOGORO WA SHAMBA LA MANYARA RANCH KWA KUKABIDHI HATI KWA MKURUGENZI WA HALMASHAURI YA WILAYA YA MONDULI


WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amemaliza mgogoro wa ardhi  uliodumu kwa miaka 17 kati ya vijiji viwili vya Ortukai na Esilalei na Taasisi ya Tanzania Land Conservation Trust (TLCT) baada ya kukabidhi hati ya  shamba la Manyara Ranch  kwa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Monduli, Stephen Ulaya.

Hati hiyo imetolewa jana jioni (Jumapili, Desemba 4, 2016) na Waziri Mkuu katika mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye kata ya Mto wa Mbu kwenye viwanja vya Barafu baada ya kubadilishwa umiliki wa shamba hilo kwenda kwa wananchi wa vijiji  hivyo vilivyopo kwenye  Kata ya Elesilalei Wilayani Monduli Mkoani Arusha.

Hatua hiyo imekuja baada ya kilio cha muda mrefu cha wananchi hao kudai kuwa Rais wa Awamu ya tatu, Benjamin Mkapa aliagiza shamba hilo ligaiwe kwa wananchi hao lakini jambo hilo halikufanyika na badala yake watu wachache walijimilikisha shamba hilo kinyemela chini ya wenyekiti wa bodi ya TLCT.

Waziri Mkuu alisema Serikali imeamua kurudisha umiliki wa shamba hilo kwa wananchi wa vijiji hivyo viwili baada ya Baraza la Madiwani na Uongoziwa Wilaya hiyo ya Monduli kuridhia kwa pamoja umiliki huo kurudi kwa wananchi kama ilivyoamriwa hapo awali.

"Shamba hili lenye ukubwa wa ekari 44,930 sasa si mali tena ya Taasisi ya Tanzania Land Conservation Trust (TLCT) iliyokuwa inafadhiliwa na Shirika la African Wildlife Foundation (AWF) sasa ni mali ya wananchi na halmashauri ya wilaya ya Monduli ndio itapanga matumizi bora ya ardhi ya shamba hili mliloteseka nalo kwa muda mrefu ," alisema.

Alisema nyaraka zinazoonyesha kuwa shamba hilo lililotolewa kwa wananchi wa vijiji vya Elesilalei na Ortukai na Rais Mstaafu wa awamu ya tatu mwaka 1999 kwa ajili ya kilimo na ufugaji lakini jambo hilo  halikufanyika badala yake taasisi ya TLCT ikajimilikisha shamba hilo kinyume na maagizo.

Hata hivyo Waziri Mkuu alisema Serikali inaendelea kufuatilia maeneo yote yaliyochukuliwa na watu bila ya kuyaendeleza na kuwapa wananchi. "Ni kwa nini watu wenye fedha wanachukua mashamba mkubwa bila ya kuyaendeleza huku wananchi wakiteseka kwa kukosa maeneo ya kilimo na ufugaji," alisema.

Awali kabla ya kuhutubia mkutano huo wa hadhara Waziri Mkuu alitembelea shule ya msingi ya Laiboni iliyoanzishwa  na mzee maarufu wa kimila wilaya huko Laigwanani Meshuko Ole Mapii ambayo inawanafunzi 102 wakiwemo wajukuu na watoto wa mzee  ambapo alitangaza umiliki wa shamba hilo kurudi kwa wananchi.

Kwa upande wake Naibu Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi, Mheshimiwa William Ole Nasha alisema wizaraya yake itaendelea kutekeleza Sera za Kilimo nchini pamoja na kusimamia matumizi bora ya ardhi kwenye shamba hilo kutokana na ukosefu mkubwa ardhi kwa ajili ya wafugaji na wakulima.

“Nikuhakikishie Mheshimiwa Waziri Mkuu kuwa tutaendelea kuhakikisha wananchi wafanya ufugaji wa kisasa wenye kwa tija kwa kutumia shamba hili. Pia nakupongeza Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa kutekeleza ilani ya Chama Cha Mapinduzi kwa vitendo na maagizo uliyotupa ya kuhakikisha wananchi wanatumia ardhi hiyo vizuri tutayasimamia,” alisema.

Baada ya shamba hilo kurudishwa kwa wananchi Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Bw. Mrisho Gambo alisema ‘’Nashukuru leo umiliki wa shamba hili umebadilishwa na naishukuru Serikali yangu tulivu kwa kutoa hati hii kwa Mkurugenzi  wa wilaya ya Monduli ili wananchi waweze kunufaika na ardhi yao na sio watu wachache wanaolipwa mamilioni ya fedha bila ya sababu za msingi’’.

Naye Waziri wa Maliasili na Utalii, Mheshimiwa Jumanne Maghembe aliwasihi wananchi hao kuheshimu njia za mapito ya wanyama (ushoroba) katika eneo hilo ambalo wanyamapori kutoka hifadhi za Tarangire, Manyara na Ngorongoro wanalitumia kwa ajili ya kupita kwenye hifadhi hizo mara kwa mara.

Katika hatua nyingine Waziri Mkuu amempa siku mbili Mkuu wa Idara ya Ardhi na Mazingira wa wilaya ya Monduli , Adil Mwanga kumuondoa muwekezaji, Lekisongo Meijo katika shamba lenye ukubwa wa ekari 2,800 lililoko katika kijiji cha Lemoti tarafa ya Kisongo ambalo alimilikishwa bila ya kufuata taratibu na kulirudisha kwa wananchi.

Pia amemuagiza Mkuu wa Mkoa wa Arusha Bw. Gambo kufanya uchunguzi wa umiliki wa mashamba mengine makubwa ambayo yana migogoro na  hayajaendelezwa mkoani humo likiwemo la Makuyuni Stein Seed Valley na  kuipatia  ufumbuzi migogoro hiyo.


EmoticonEmoticon

Note: Only a member of this blog may post a comment.