Sunday, December 18, 2016

NASSARI ASIFU UTENDAJI WA SERIKALI YA AWAMU YA TANO

*Aja nchini kwa dharura kutoka masomoni Uingereza ili kumuwahi Waziri Mkuu

MBUNGE wa jimbo la Arumeru Mashariki, Mheshimiwa Joshua Nassari amepongeza na kusifu  jitihada kubwa zianazofanywa na Serikali ya Awamu ya Tano katika kuwaletea maendeleo wananchi wa maeneo mbalimbali nchini wakiwemo wa jimbo lake.

Kufuatia hatua hiyo Mheshimiwa Nassari ameahidi kushirikiana bega kwa bega na Serikali ili kuhakikisha maendeleo yanakuwa endelevu. Mheshimiwa Nassari ametoa pongezi hizo leo (Jumapili, Desemba 18, 2016) mbele ya Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ambaye alikuwa katika majumuisho ya ziara yake ya siku 10 ya kikazi mkoani Arusha.

Mbunge huyo ambaye alilazimika kuja nchini kwa dharura akitokea masomoni nchini Uingereza ili kumuwahi Waziri Mkuu, amesema ameridhishwa na hatua za utatuzi wa migogoro ya ardhi zinazochukuliwa na Serikali.

Amesema ziara ya Waziri Mkuu mkoani Arusha, imesaidia kutibu majeraha na makovu makubwa yalitokana na matokeo ya uchaguzi mkuu wa mwaka jana."Kama kuna kiongozi ambaye hawezi kuunga mkono jitihada hizi za kuwaletea maendeleo watu wetu, atakuwa na matatizo,” amesema.

Ameongeza kuwa kitendo cha Waziri Mkuu kuweka mikakati ya kushughulikia migogoro ya ardhi iliyodumu kwa miaka mingi ni ushahidi tosha kwamba Serikali ya Awamu ya Tano imedhamiria kuwasaidia wananchi wa kawaida.

Mheshimiwa Nassari amesema mwaka 1952 wazee wa Meru walimtuma mtu kwenda Uingereza kuomba uhuru wa wananchi wa Arumeru ili waweze kujitawala na kumiliki ardhi yao kutoka kwa wakoloni.

Amesema wazee hao walichukua uamuzi huo baada ya kuchoshwa na vitendo vya unyanyasaji vilivyokuwa vinafanywa na wakoloni dhidi yao. Lakini miaka 55 imepita tangu nchi ipate Uhuru bado migogoro na mateso hayo yapo.

Hivyo amempongeza Waziri Mkuu kwa kuamua kuitafutia ufumbuzi changamoto ya ardhi wilayani Arumeru jambo ambalo litawawezesha wananchi kupata ardhi kwa ajili ya kuendesha shughuli zao za kimaendeleo zikiwemo za  kilimo na ufugaji.

Waziri Mkuu jana (Jumamosi, Desemba 17, 2016) alifanya ziara katika wilaya ya Arumeru ambapo alisema Serikali itawanyang’anya ardhi wamiliki wote wa mashamba makubwa wilayani Arumeru ambao hawajayaendeleza kwa sababu wamekiuka mkataba wa umiliki.

Alisema Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Mheshimiwa William Lukuvi atakuja mkoani Arusha kwa ajili ya kufanya mapitio ya mashamba yote makubwa ambayo hayajaendelezwa na kuyarudishwa Serikalini.

 “Tufanya mapitio ya kila shamba ili kujua linamilikiwa na nani na alipewa lini na tangu alipokabidhiwa amefanya nini. Shamba lisiloendelezwa litarudisha kwa wananchi. Kama mtu ameshindwa kupata mtaji kwa muda wa miaka 10 atapata leo,” amesema.

Amesema Serikali haiko tayari kuona wananchi wakinyanyaswa kwa kukosa ardhi ya kilimo kwa sababu ya watu wachache kumiliki maeneo makubwa bila ya kuyaendeleza..

"Ninataarifa kwamba hapa Arumeru kuna baadhi ya wawekezaji wanamiliki mashamba makubwa na hawajayaendeleza. Wengine wanakodisha kwa wananchi ili kujipatia fedha kinyume na mikataba yao ya umiliki. Hatutawavumilia,” alisema.

Alisema wilaya ya Arumeru inaongoza kwa migogoro ya ardhi na maeneo mengi yametwaliwa na mtu mmoja mmoja na baadhi yao wamekuwa wakilitumia vibaya Jeshi la Polisi kwa kuwanyanyasa wananchi wanaokatiza au kulima kwenye maeneo hayo, ambapo aliwataka polisi kuacha tabia hiyo mara moja.


EmoticonEmoticon

Note: Only a member of this blog may post a comment.