*Aonyeshwa pia pembe mbili za faru huyo
WAZIRI
MKUU Kassim Majaliwa amepokea taarifa inayoelezea utaratibu uliotumika
kumhamisha faru John kutoka Hifadhi ya Ngorongoro kwenda Sasakwa Black Rhino
Sanctuary iliyoko kwenye Hifadhi ya Grumeti.
Akizungumza
katika kikao kilichofanyika nyumbani kwake Oysterbay leo mchana (Ijumaa,
Desemba 9, 2016) na kuhudhuriwa na Waziri wa Maliasili na Utalii, Prof. Jumanne
Maghembe na baadhi ya watendaji wa wizara yake, Waziri Mkuu amesema taarifa
hiyo itafanyiwa kazi na wataalamu wa ofisi yake.
“Nilipokea
taarifa yenu jana saa 7 usiku lakini nikaahidi kuwa leo tukimaliza sherehe za maadhimisho
ya Uhuru tukutane na kujadiliana kuhusu taarifa yenu,” amesema.
Akisoma
taarifa hiyo mbele ya Waziri Mkuu, Prof. Maghembe alisema hadi kufikia Desemba
2015 wakati faru John anahamishwa alikuwa na watoto 26 (sawa na asilimia 70.2)
ya faru wote waliokuwepo ndani ya kreta.
“Kati
ya faru 37 waliokuwepo ndani ya kreta, watoto wake walikuwa 26 sawa na asilimia
70.2. Uamuzi wa kumuondoa John ulikuwa ni muhimu ili kuwezesha kuongezeka kwa
faru weusi na kupunguza tatizo la ‘inbreeding’ ndani ya Hifadhi ya Ngorongoro,”
alisema Waziri Maghembe.
Baada
ya kuhamishiwa Sasakwa, Waziri Maghembe alisema Julai 10, 2016 afya ya faru
John ilianza kudorora na alikufa tarehe 18 Agosti, mwaka huu. Taarifa hiyo iliandaliwa
na Kamati ya Taifa ya Kuwalinda Tembo na Faru. Kamati hiyo inaundwa na
Mkurugenzi Mkuu wa TAWIRI, Mkurugenzi Mkuu wa TANAPA, Mkurugenzi Mkuu wa NCAA
na Mhifadhi Mkuu wa Ngorongoro.
Akikabidhi
pembe za faru huyo mbele ya Waziri Mkuu, Kaimu Mkurugenzi Msaidizi wa Kitengo
cha Kupambana na Ujangili wa Wanyamapori, Bw. Robert Mande alimweleza kwamba
pembe kubwa ya faru John ilikuwa na uzito wa kilo 3.6 na pembe ndogo ilikuwa na
uzito wa kilo 2.3.
Watendaji
wa wizara waliohudhuria kikao hicho ni Kaimu Katibu Mkuu, Bw. Iddi Mfunda; Mhifadhi
Mkuu wa Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA), Bw. Freddy Manongi; Mkurugenzi
Mkuu wa TAWIRI, Bw. Simon Mduma; Kaimu Mkurugenzi Idara ya Wanyamapori, Bw.
Alexander Songorwa na Mkuu wa Pori la Akiba la Ikorongo/Grumeti, Bw. Nollasco
Ngowe.
Desemba
6, mwaka huu, akiwa ziarani mkoani Arusha, Waziri Mkuu aliuagiza uongozi wa
Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA), umletee nyaraka zote zilizotumika kumhamisha
faru maarufu kwa jina la ‘John’ kutoka kwenye hifadhi hiyo ifikapo Alhamisi, Desemba
8.
Alitoa
agizo hilo alipotembelea ofisi za makao makuu ya NCAA zilizoko wilayani
Ngorongoro, mkoani Arusha na kuzungumza na watumishi wa mamlaka hiyo pamoja na
Wajumbe wa Baraza la Wafugaji ikiwa ni sehemu ya ziara yake ya kikazi mkoani humo.
EmoticonEmoticon
Note: Only a member of this blog may post a comment.