WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amelazimika kuendesha harambee ya papo kwa papo ma kuchangisha sh.milioni 138.26 ili kufanikisha ujenzi wa shule mpya ya sekondari wilayani Ruangwa.
Hatua hiyo hiyo inafuatia wingi wa wanafunzi waliofaulu mtihani wa darasa la saba na kuchaguliwa kuingia kidato cha kwanza lakini hawakufanikiwa kupata nafasi katika mkupuo wa kwanza.
“Katika kikao cha Halmashauri ya Wilaya cha hivi karibuni ilionekana kuna haja ya kujenga shule mpya ya sekondari ili kukabiliana na wingi wa watoto waliofaulu mtihani wa darasa la saba na kuchaguliwa kuingia kidato cha kwanza. Tunawashukuru sana wenzetu ambao wametoa maeneo yao bure ili shule ijengwe haraka,” amesema.
Katika harambee iliyofanyika kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika mjini Ruangwa leo mchana (Ijumaa, Desemba 30, 2016), Waziri Mkuu amefanikisha kupatikana kwa fedha kiasi cha sh. milioni 120.65 na mifuko 550 ya saruji na mabati 360 (vyenye thamani ya sh. milioni 17.61) ambavyo vitatumika kujenga madarasa manne ya kidato cha kwanza yanayotakiwa kuwa yamekamilika ifikapo Januari 15, 2017.
Kwa mujibu wa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Ruangwa, Bw. Andrea Chezue, jumla ya watoto 319 walichaguliwa kujiunga na kidato cha kwanza lakini walikosa nafasi sababu ya ukosefu wa madarasa na walitakiwa kusubiri hadi chaguo la pili ambalo kwa kawaida hufanyika Februari, kila mwaka.
“Wanafunzi waliofaulu na kukosa nafasi jumla yao ni 319 lakini kwa hapa Ruangwa mjini ni 179 na waliobakia 140 wanatoka kwenye kata za jirani za Nachingwea na Mandarawe. Shule hii ya sekondari itahudumia kata tatu. Kwa hiyo Halmashauri imepanga kujenga madarasa manne hapa mjini ili watoto wote waweze kuanza mara moja,” amesema.
Mkurugenzi huyo amesema ili kupunguza tatizo hilo mwakani, wataendeleza ujenzi wa madarasa manne manne waweze kuwa na mikondo minne kwa kila kidato. “Halmashauri ya Ruangwa imetenga sh. milioni 75, wananchi wa Kata ya Ruangwa wametoa sh. milioni 1.2 na wananchi wa kata ya Nachingwea wametoa sh. milioni 2.25,” amesema.
Waziri Mkuu ambaye ni mbunge wa jimbo hilo, amechangia sh. milioni 33 kutoka kwenye mfuko wa jimbo ili kuharakisha ujenzi wa madarasa mawili ya kuanzia. Wengine waliochangia harambee hiyo ni kampuni ya Paco Gems Ltd, (sh. milioni 6), Baraka Solar (sh. milioni moja), Ofisi ya Mkuu wa Mkoa (sh. milioni 1), Kampuni ya Asamalema (sh. milioni 1) na mfanyabiashara wa Ruangwa, Bw. Abdallah Namkudai (sh. 200,000).
Wengine ni kampuni ya wanyumbani construction mifuko 100 ya saruji, kampuni ya Lindi Jumbo (mabati 100 na mifuko 100 ya saruji), kampuni ya madini ya Nazareth (mifuko 150 ya saruji), kampuni ya URANEX inayochimba madini ya Graphite (mabati 260), mgodi wa dhahabu wa Namungo (mifuko 100 ya saruji) na Kampuni ya ujenzi ya Nahungo Construction Ltd. (mifuko 100 ya saruji).
Waziri Mkuu amewashukuru wote waliojitolea kuchangia ujenzi wa shule hiyo. Amerejea jijini Dar es Salaam jioni hii.
EmoticonEmoticon
Note: Only a member of this blog may post a comment.