Wednesday, December 28, 2016

RC ATOA WIKI MBILI WANANCHI WAJENGE VYOO

*Msako wa DC kupita Jan. 15 mwakani
*Asiye na choo kutozwa faini ya sh. 50,000

MKUU WA MKOA wa Lindi, Bw. Godfrey Zambi ametoa wiki mbili kwa wakazi wa jimbo la Ruangwa kuhakikisha kuwa wanajenga vyoo ili kujiepusha na ugonjwa wa kipindupindu.

Amemtaka Mkuu wa Wilaya ya Ruangwa, Bw. Joseph Mkirikiti afanye msako wa nyumba kwa nyumba ifikapo Januari 15, 2017 na endapo atakuta kuna mkazi wa kijiji chochote hajajenga choo, basi atozwe faisi ya sh. 50,000 mara moja.

Ametoa a leo (Jumatano, Desemba 28, 2016) wakati akizungumza na wananchi wa vijiji vya Namilema, Mbuyuni, Nandandara, Namkonjera, Muhuru, Chikundi na Chibula wilayani humo ambako alikuwa akiwasalimia wananchi kabla ya kumkaribisha Waziri Mkuu azungumze na wakazi wa vijiji hivyo.

Waziri Mkuu yuko Ruangwa kwa siku nne kwa mapumziko ya mwisho wa mwaka na ameamua kutumia muda huo kuwasalimia wananchi wa jimbo lake na kuhimiza kazi za maendeleo.

Mkuu huyo wa Mkoa amesema wakulima wengi wamevuna korosho msimu na baadhi yao wamelipwa vizuri, hivyo hawana budi kutumia sehemu ya fedha hizo kujenga vyoo ili kujiepusha na magonjwa ya mlipuko na hasa kipindupindu.

“Hili ni agizo la Serikali siyo yangu binafsi kwa hiyo ni amri halali. Kikilipuka kipindupindu, naanza na Mkuu wa Wilaya kabla na mimi sijaulizwa na Mheshimiwa Waziri Mkuu au Mheshimiwa Rais,” amesema.

Katika hatua nyingine, Bw. Zambi amewahimiza wakazi wa vijiji hivyo wapande miche ya mikorosho katika msimu huu wa kilimo pindi mvua zitakapoanza kwani iliyopo imekaa kwa zaidi ya miaka 50 na sasa haizai matunda ya kutosha.

“Mkoa wetu una mpango wa kubadilisha miti ya mikorosho kwani mingi ni ya zamani na imelkaa kwa zaidi ya miaka 40 hadi 50 na hivi sasa haina tija kwenye mazao yake. Mti mzuri wa korosho unazaa hadi kilo 40 lakini hii iliyopo sasa hivi inatoa kilo 10 tu,” amesema.

Amesema Serikali imeagiza kila kijiji kiandae miche 5,000 kwa mwaka na kuwapa wananchi kwa bei nafuu na mpango huo tumeshaanza kuutekeleza.


EmoticonEmoticon

Note: Only a member of this blog may post a comment.