Wednesday, September 25, 2019

KILIMO, MIFUGO NA UVUVI KUCHANGIA UCHUMI-MAJALIWA


WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema Serikali ya awamu ya tano inayoongozwa na Rais Dkt. Magufuli itaendelea kuhakikisha kuwa kilimo, ufugaji na uvuvi unakuwa wa kisasa na wenye tija kwa wananchi sambamba na kutoa mchango unaostahili katika kufikia uchumi wa kati unaoongozwa na viwanda ifikapo mwaka 2025.

“Katika kuhakikisha azma hiyo ya Serikali inafikiwa, nitoerai kwa wafugaji nchini kuunda ushirika imara utakao wawezesha kupata huduma mbalimbali za mifugo na ushirika huo pia ulenge katika kuboresha uzalishaji na ukusanyaji wa maziwa, upatikanaji wa masoko pamoja na kuongeza kiasi cha usindikaji viwandani. 

Waziri Mkuu ameyasema hayo leo (Jumatano, Septemba 25, 2019)kwenye Maadhimisho ya Siku ya Unywaji Maziwa Shuleni yaliyofanyika katika Viwanja vya Mwembetogwa mijini Iringa. “Unywaji maziwa shuleni si tu ni muhimu lakini pia inatoa msukumo wa kuboresha afya zetu hususan za watoto shuleni kupitia unywaji wa maziwa.”

Amesema wataalamu wa lishe wanashauri kula chakula bora kinachokuwa na viini lishe vyote muhimu kama wanga, protini, vitamini, madini, mafuta na maji ya kutosha. Hata hivyo, ili kupata chakula bora, wananchi wanapaswa kuchanganya vyakula vya aina nyingi katika mlo mmoja.

Waziri Mkuu amesema kutokana na umuhimu huo, ndiyo maana watalaamu wa lishe wanashauri kuwa mtoto apate glasi moja ya maziwa katikati ya siku itakayompatia lishe ya kutosha hadi atakapomaliza masomo yake kwa siku hiyo. “Kwa bahati mbaya hapa nchini, watoto wengi huondoka asubuhi kwenda shuleni bila kupata chakula chochote. Aidha, shuleni nako mara nyingi hawapati chakula na hivyo hukosa usikivu mzuri katika masomo yao.”

Zaidi ya nchi 70 duniani ikiwemo Tanzania zinaadhimisha siku ya unywaji maziwa na tayari zilishaanzisha mpango wa unywaji maziwa shuleni kwa watoto wao, lengo ni kuhakikisha mtoto anapata lishe kamili na anakuwa na usikivu mzuri katika masomo yake. Mtoto amelengwa kwa sababu ni kundi ambalo ni muhimu katika kujenga Taifa lililo bora na anatarajiwa kurithisha vema vizazi vijavyo.

“Nimearifiwa kuwa hapa nchini programu ya unywaji maziwa shuleni ilianza kutekelezwa katika  mikoa ya Arusha, Kilimanjaro, Tanga, Morogoro, Iringa, Dar es Salaam na Njombe ambapo shule 40 na wanafunzi 34,561wamenufaika katika kunywa maziwa lita 631,860 ambayo yamekuwa yakitolewa kwa ushirikiano na Serikali, wazazi, wafadhili mbalimbali na wasindikaji wa maziwa. Lengo kuwafikia wanafunzi wote.”

Waziri Mkuu amesema Serikali ina nia ya dhati ya kufanya mpango huu uwe wa kitaifa. Serikali kupitia Wizara ya Mifugo na Uvuvi ikishirikiana na wadau wengine itaendelea kuhamasisha unywaji wa maziwa katika shule zetu hapa nchini.  Juhudi hizi zitakwenda sambamba na kuongeza uzalishaji wa maziwa kutoka lita  bilioni 2.7 zinazozalishwa sasa kwa mwaka mpaka lita bilioni saba kwa mwaka ifikapo 2020.

Waziri Mkuu ametumia fursa hiyo kuwapongeza wafugaji wa Iringa kwa kuwa mfano mzuri wa kuigwa kwa mafanikio yanayoonekana katika kuendeleza tasnia ya maziwa kupitia ushirika. “Nitoe wito kwa Mamlaka za Serikali za Mitaa kuhakikisha zinawezesha na zinasimamia uundwaji wa vyama vya ushirika imara na pia kuimarisha vyama vya ushirika vilivyopo.”

Maadhimisho hayo yamehudhuriwa na Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi William Lukuvi, Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Josephat Kandege, Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi anayeshughulikia mifugo, Profesa Elisante Ole Gabriel, Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Maafisa wa Serikali, wadau wa mazima pamoja na wananchi.


 (mwisho)


EmoticonEmoticon

Note: Only a member of this blog may post a comment.