Friday, September 27, 2019

RC FUATILIA UTENDAJI KAZI OFISI YA DC KILOLO-MAJALIWA


WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amemwagiza Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Ally Happi afuatilie utendaji kazi kwenye ofisi ya mkuu wa wilaya ya Kilolo kufuatia watumishi 14 wa ofisi hiyo wakiwemo madereva 10 kuhamishwa baada ya Mkuu wa Wilaya hiyo Asia Abdallah kudai kuwa hawafanyi kazi ipasavyo.
Hata hivyo, Waziri Mkuu amesema ni mhuimu kwa viongozi wakatambua dhamana zao katika utekelezaji wa shughuli zao pamoja na kuwatambua, kuwajali na kuwathamini watumishi wa kada zote wakiwemo madereva, hivyo ni vizuri wawaandae kwa kuwapa maelekezo kwa wakati kwa kuwa nao ni binadamu na wanafamilia.
Waziri Mkuu ametoa agizo hilo leo (Ijumaa, Septemba 27, 2019) wakati akizungumza na watumishi wa wilaya ya Kilolo, Halmashauri ya wilaya ya Kilolo pamoja na Madiwani wa Halmashauri hiyo akiwa katika siku ya nne ya ziara yake ya kikazi mkoani Iringa. Amesisitiza umuhimu wa watumishi hao kushirikiana.
Waziri Mkuu amesema pamoja na shughuli za maendeleo wanazofanya katika wilaya hiyo lakini hawana mshikamano, hivyo amemtaka Mkuu wa Wilaya ahakikishe anashirikiana vizuri na wenzake kwa sababu watumishi wengi wamehamishwa tangu aingie katika ofisi hiyo na hata wanaoletwa wanalalamika na wanaomba wahamishwe.
Amesema watumishi wengi katika ofisi hiyo anawaona hawana uwezo wakiwemo wasaidizi wake kama madereva, watunza kumbukumbu na makatibu muhtasi. “Hata aliyekuwa Katibu Tawala wa wilaya hii alihamishwa kwa sababu na kutoelewana na DC, na hata huyu Katibu Tawala wa Wilaya aliyepo sasa hana raha anataka kuhama kwa sababu hizo hizo.”
“Lazima tuwatambue wasaidizi wetu na majukumu yao. Ofisi ya Mkuu wa Wilaya haiwezekani ikawa hivi, lazima kuna shida kuwaondoa watumishi wote, Mkuu wa Mkoa fuatilia hii ni mpya. Hapa tujue mbovu ni nani Mkuu wa Mkoa tunataka tujue DC wako anataka dereva wa aina gani, tangu amefika hapa madereva 10 wote hawafai? 
Waziri Mkuu ameongeza kuwa “ili mfanye kazi vizuri mnatakiwa mshikamane mfanye kazi kama timu moja kwani pamoja na shughuli mnazofanya hamna ushirikiano. DC (mkuu wa wilaya) sasa utabaki peke yako utakuwa unaandika mwenyewe, unaendesha gari mwenyewe maana wote hawafai. Mkuu Mkoa nakukabidhi majina ya watumishi hao ushughulikie suala hili. Na Katibu Tawala wa Mkoa usilete watumishi wengine hapa mpaka suala hili litakapopatiwa ufumbuzi”
Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu ameziagiza halmashauri zote nchini zihakikishe zinatenga kiasi cha fedha katika makusanyo yao ya ndani kwa ajili ya kutekeleza ujenzi wa miradi ya kimkakati kwenye maeneo yao kama ujenzi wa vituo vya afya, barabara za halmashauri na masoko badala ya kutegemea fedha kutoka Serikali Kuu pekee.
Amesema wilaya ya Kilolo ambayo haina kituo cha mabasi inatakiwa itenge fedha kutoka kwenye makusanyo yao na kuanzisha mradi wa kituo hicho ambao utekelezaji wake utaboresha huduma kwa wananchi pia, mradi huo utasaidia katika kuongeza mapato ya halmashauri. Halmashauri ya wilaya ya Kilolo inakusanya sh. bilioni nne kwa mwaka.
Waziri Mkuu amesema watumishi wanapaswa kutekeleza majukumu yao ipasavyo kwani wananchi wanahitaji waone matokeo ya uwepo wao kutokana na dhamana waliyotewa na Serikali katika wilaya hiyo. “Madiwani nanyi simamieni halmashauri yenu vizuri kwa sababu nyie ndiyo wenye dhamana ya kuhakikisha wananchi wanahudumiwa vizuri.”
Awali, Mbunge wa jimbo la Kilolo, Venance Mwamoto aliishukuru Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Rais Dkt. John Magufuli kwa kutoa fedha za utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo katika wilaya yao ikiwemo ya umeme, ambapo kati ya vijiji 94 vilivyoko vijiji 54 vimeunganishiwa huduma hiyo na vilivyosalia vitakuwa viunganishiwa umeme ifikapo Desemba mwaka huu.
Akizungumzia kuhusu miradi ya maji mbunge huyo alisema kati ya vijiji 94 vya wilaya hiyo vijiji 15 tu ndio bado havina maji ya uhakika lakini wanaendelea na mchakato wa ufuatiliaji ili kuhakikisha navyo vipata maji safi na salama.”Kuhusu sekta ya elimu tatizo tulilonalo ni madai ya walimu waliohama na waliopandishwa madaraja.” Waziri Mkuu amesema suala hilo linafanyiwa kazi.
Mapema, Waziri Mkuu alikagua mradi wa ujenzi wa hospitali ya wilaya na kupokea taarifa ya ujenzi wa hospitali hiyo ambapo alisema ameridhishwa na ujenzi huo uliogharimu sh. bilioni nne na alitumia fursa hiyo kuwapongeza viongozi wa wilaya hiyo akiwemo Mkurugenzi pamoja na mkandarasi anayenga.

(mwisho)


EmoticonEmoticon

Note: Only a member of this blog may post a comment.