Thursday, September 12, 2019

TOZENI BILI ZA MAJI ZISIZOWAUMIZA WANANCHI-MAJALIWA


WAZIRI MKUU, Kassim Majaliwa ameiagiza Wizara ya Maji ifuatilie utendaji wa Mamlaka zilizopewa dhamana ya kusimamia miradi ya maji katika maeneo mbalimbali nchini na ihakikishe kwamba bili wanazotozwa wananchi zinakuwa na uhalisia na si kuwaumiza.
Ametoa agizo hilo baada ya kuibuka wimbi la malalamiko kutoka kwa wananchi kuhusu upandaji wa bili za maji ambao hauna uhalisia kwa sababu Serikali ndiyo inayotoa fedha za miradi hiyo nchini.”Serikali haitakubali wala haitoruhusu mwananchi anatozwa gharama kubwa za maji.”
Waziri Mkuu ameyasema hayo leo (Alhamisi, Septemba 12, 2019) Bungeni jijini Dodoma katika kipindi cha maswali ya papo kwa papo kwa Waziri Mkuu wakati akijibu swali la Mbungewa Viti Maalumu, Mariam Kisangi, aliyetaka kujua kauli ya Serikali kuhusu suala hilo.
“Yako maeneo ambayo mamlaka zilizopewa dhamana ya kusimamia miradi ya maji kumejitokeza wimbi la mabadiliko ya kuhusu kupanda kwa bei za bili, mfano wilayani Maswa mkoani Simuyu bei imeongezeka kutoka sh. 5,000 hadi 28,000 kwa mwezi.”
“Bei hizo hazina uhalisia na hakuna sababu ya mamlaka kuzoza bei kubwa kiasi hicho na kuwafanya wananchi washindwe kumudu kulipia bili zao, wakati Serikali ndio imetoa fedha za kugharamamia uanzwishwaji wa miradi hiyo na haijadai kurudishiwa fedha hizo.”
Waziri Mkuu amesema Wizara ya Maji kupitia Mamlaka ya Udhibiti wa Nishati na Maji (EWURA) ifuatilie bei za bili wanazotozwa wananchi ili kujiridhishwa kwamba zinazingatia uwezo wa wananchi wengi kuzilipa hasa wale wa vijijini.
Wakati huo huo, Waziri Mkuu amewaagiza Wakuu wa Mikoa, Wilaya, Wakurugenzi wa Halmashauri, Maafisa Kilimo na Maafisa Biashara kote nchini wasimamie katika masoko yote na wajirishe iwapo vipimo vinavyotumika ni sahihi kwani lumbesa haikubaliki.

Ametoa agizo hilo wakati akijibu swali la Mbungewa Jimbo la Mlalo, Rashid Shangazi aliyetaka kupata kauli ya Serikali kuhusu hatua zilizochukuliwa katika kudhibiti unyonyaji wanaofanyiwa wakulima kupitia ufungaji wa mazao unaozidi viwango.

Waziri Mkuu amesema wanunuzi wa mazao mbalimbali lazima wafuate sharia, kanuni na taratibu za manunuzi ya mazao husika. “Maafisa Kilimo wasimamie biashara hiyo na waendeshe operesheni kwenye maeneo ya masoko ili kujirishana vipimo vinavyotumika.”

Amesema ni muhimu zaidi kutumia mizani ambayo haina utata ili kuwawezesha wakulima kuweza kunufaika kutokana na kilimo na kwamba suala la waununuzi kutumia vipimo visivyosahihi kama lumbesa halikubaliki.
Akijibuswali la Mbunge wa Sumve, Richard Ndasa aliyetaka kupata kauli ya Serikali kuhusu kuhusu suala la ununuzi wa zao la pamba, Waziri Mkuu amesema Serikali imelifanyia kazi suala hilo na tayari zaidi ya tani 200,000 zimeshanunuliwa ambayo ni sawa na asilimia 80.
Waziri Mkuu amewahakikishia wakulima wa zao la pamba kwamba pamba yote iliyosailia majumbani itanunuliwa. 
(mwisho)


EmoticonEmoticon

Note: Only a member of this blog may post a comment.