Tuesday, September 17, 2019

SIJARIDHISHWA NA GAWIO LINALOTOLEWA NA KIWANDA CHA KILOMBERO-MAJALIWA

 
WAZIRI MKUU Kassimu Majaliwa amesema hajaridhishwa na gawio la shilingi milioni 800 linatolewa na kiwanda cha Sukari cha Kilombero ambacho uzalishaji wake ni kikubwa ikilinganishwa na kiwanda cha sukari cha Moshi TPC ambacho kinatoa gawio la sh. billion 15 kwa mwaka.

Waziri Mkuu ameyasema hayo leo (Jumanne, Septemba 17, 2019) wakati alipotembelea kiwanda hicho, akiwa katika siku ya nne ya ziara yake ya kikazi Mkoani Morogoro. Amevitaka viwanda vya sukari nchini kuzaliza sukari ya kutosha ili kukidhi mahitaji.

Akizungumzia kuhusu vibali vya uagizaji wa sukari, Waziri Mkuu amesema Serikali iliamua kutoa nafasi ya kuagiza sukari kwa wenye viwanda ili kuepuka ujanja uliokuwa ukifanywa na baadhi ya wafanyabiashara ambao walikuwa wakiagiza sukari kutoka nje ya nchi ambayo nyingine ilikuwa haina ubora.

Hata hivyo, Waziri Mkuu amesema Tanzania bado kuna uhitaji mkubwa wa sukari hususani ya viwandani, hivyo kusababisha Serikali kutoa vibali kwa wamiliki wa viwanda kuagiza sukari kutoka nje ya nchi. “Viwanda vya ndani vya sukari vihakikishe vinaongeza uzalishaji wa sukari ya viwandani ili kukabiliana na upungufu uliopo.

Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Kilimo, Omary Mgumba amesema mahitaji ya sukari kwa mwaka huu nchini yameongezeka hadi kufikia tani 710,000 ikilinganishwa na tani 610,000 za mwaka jana.

Amesema ongezeko hilo limechangiwa na kuongezeka kwa viwanda vipya vinavyotumia sukari ya viwandani, ambapo kwa sasa mahitaji ya sukari ya viwandani yamefikia tani 165,000. 

Amesema mahitaji ya sukari za majumbani kwa sasa ni tani 545,000, ambapo kiwanda cha Kilombero kinazalisha tani 134,000, kiwanda cha Manyara tani 6,000, kiwanda cha Mtibwa tani 39,000 na TPC cha Moshi tani 100,000.

Naibu Waziri huyo amesema ili kukabiliana na upungufu wa sukari Serikali imeweka mkakati wa kuanzishwa kwa viwanda vipya vya sukari vya Bagamoro ambacho kitaanza kuingiza awamu ya kwanza ya sukari sokoni tani 35,000 ifikapo mwaka 2022 na kiwanda cha Mkulazi kinatarajiwa kuzalisha tani 200,000 na cha Mbigili tani 50,000.

Akitoa taarifa za kiwanda hicho Mwenyekiti wa Bodi ya Sukari Balozi Amry amesema Kampuni ya Sukari ya Kilombero imezingatia kikamilifu wito wa Serikali wa kukuza uzalishaji na kuweka mipango thabiti ya upanuzi wa uzalishaji wa kilimo cha miwa na kiwanda cha kusindika miwa. Mradi huo utagharimu sh. bilioni 700.

Katika hatua nyingine,Waziri Mkuu ametoa muda wa wiki mbili kwa Mkurugenzi wa Halmashauri ya wilaya ya Kilosa awe amechimba visima katika kata ya Ruaha kwa ajili ya kuwawezesha wakazi wa eneo hilo kupata maji safi na salama.

Ameyasema hayo baada ya wakazi wa kata hiyo kusimamisha msafara alipokuwa akielekea kata ya Malolo. Amesema halmashauri hiyo inakusanya zaidi ya sh. bilioni mbili kwa mwaka hivyo inatakiwa kutenga kiasi cha fedha za mapato kugharamia miradi ya maendeleo ya wananchi.

Waziri Mkuu amesemaSerikali inatekeleza Kampeni ya Rais Dkt. John Magufuli ya kumtua mama ndoo kichwani, ambayo inalenga kuwaondolea wananchi tatizo la upatikanaji wa huduma ya maji safi na salama kwa kuhakikisha huduma hiyo inapatikana karibu na maeneo yao.


(mwisho)


EmoticonEmoticon

Note: Only a member of this blog may post a comment.