WAZIRI MKUU, Kassim Majaliwa ameipongeza timu ya kandanda ya Taifa, Taifa Stars kwa kufanikiwa kuiondoa Harambee Stars katika mashindano ya CHAN 2020 na kuiondoa Burundi na kufanikiwa kuingia hatua ya makundi ya kufuzu Kombe la Dunia huko Doha, Qatar 2022.
Pia, Waziri Mkuu ameipongeza timu ya Taifa ya Wanawake chini ya Umri wa Miaka 20 (Maarufu Tanzanite) kwa kutwaa kombe la mpira wa Miguu kwa Nchi za COSAFA huko Port Elizabeth, Afrika ya Kusini.
Waziri Mkuu ametoa pongezi hizo leo (Ijumaa, Septemba 13, 2019) , wakati akiahirisha mkutano wa 16 wa Bunge la 11, Bungeni jijini Dodoma. Amesema hatua hiyo ni nzuri na muhimu kwani inaiweka timu katika nafasi nzuri kushiriki fainali za mashindano hayo.
Amesema timu ya Taifa itarudi dimbani kupambana na Sudan tarehe 22 Septemba, 2019 kwenye Uwanja wa Taifa. “Kama kawaida yetu twenda tukaujaze Uwanja wetu wa Taifa na kuishangilia kwa nguvu timu yetu ya Taifa.”
Vilevile, Waziri Mkuu amevipongeza vilabu vya Azam, Malindi na Yanga kwa kufanikiwa kusonga mbele kuingia hatua ya pili katika michuano ya vilabu ya Shirikisho la Soka Barani Afrika (CAF).
“Kwa vilabu vya KMC, KMKM na Simba, ambavyo vimeondolewa katika hatua ya mwanzo kabisa, vichukulie hali hiyo kama changamoto ya kujitathmini na kujiandaa kwa ajili ya michezo ya ndani na mashindano yajayo ya kimataifa badala ya kutumia muda mrefu kujadili kuhusu kutolewa mapema.”
Akizungumzia kuhusu mchezo wa masumbwi, Waziri Mkuu amesema bendera ya Tanzania imeendelea kupeperushwa vyema kufuatia wana masumbwi wengine wawili wa Kitanzania kuendelea kufanya vizuri katika medani za Kimataifa.
“Nitumie nafasi hii kuwapongeza mwanamasumbwi Abdallah Shaaban Pazi maarufuDullaMbabe kwa kufanikiwa kutwaa ubingwa wa Dunia wa WBO baada ya kumpiga kwa knockout kwenye raundi ya tatu mpinzani wake Mchina anayejulikana kwa jina la Zulipikaer Maimaitiali.”
Pia, Waziri Mkuu amempongeza mwanamasumbwi mwingine wa Kitanzania Bruno Tarimo (maarufuvifuaviwili) kwa kumnyoosha mpinzani wake Mserbia, Scheka Gurdijeljac kwenye pambano la ubingwa wa Dunia lililofanyika mwanzoni mwa mwezi huu huko Serbia.
“Hongereni sana wanamichezo wetu na endeleeni na moyo huo wa kizalendo mliouonesha katika kuipeperusha vema bendera ya Taifa letu.”
Mbali na kuwapongeza wanamasumbwi hao, pia, Waziri Mkuu amempongezaMiss Tanzania 2019, Sylvia Bebwa pamoja na Queen Magese aliyeshika nafasi ya pili na Greatness Nkuba aliyeshika nafasi ya tatu.
“Tunamtakia matayarisho mema Miss Tanzania ili akapeperushe vema Bendera ya Taifa letu nchini Uingereza kwenye mashindano ya Urembo ya Dunia (Miss World) ambako pia ataitangaza nchi yetu na vivutio vya utalii tulivyonavyo.
Waziri Mkuu ameitaka Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo iendelee kuratibu vizuri shughuli za michezo, utamaduni na sanaa ili zilete ufanisi wa hali ya juu na pia kuweka msisitizo sambamba na kuwa na mikakati ya kuendeleza michezo ikiwemo shuleni, vituo maalumu vya michezo na kuwa na mifumo mizuri ya upatikanaji wa fedha.
(mwisho)
EmoticonEmoticon
Note: Only a member of this blog may post a comment.