WAZIRI
MKUU Kassim Majaliwa amesema ahadi zote zilizotolewa na Rais Dkt. John
Magufuli ikiwemo ujenzi wa barabara ya Mikumi-Ifakara kwa kiwango cha
lami zitatekelezwa, hivyo amewataka wananchi waendelee kuiamini Serikali
yao.
Ametoa
kauli hiyo jana (Jumanne, Septemba 17, 2019) wakati akizungumza kwa
nyakati tofauti na wananchi wa Mji wa Ifakara pamoja na wilaya ya Kilosa
alipokuwa katika siku ya nne ya ziara yake ya kikazi mkoani Morogoro.
“Kila
alichokiahidi Mheshimiwa Rais Dkt. John Magufuli nitakisimamia
kuhakikisha kinatekelezwa, hivyo wananchi endeleeni kuiamini Serikali
yenu. Serikali yenu ipo makini na ina dhamira ya dhati ya kuwaletea
maendeleo kama Ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ya 2015-2020 inavyoelekeza.”
Waziri
Mkuu alisema Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Rais Dkt.
Magufuli iko makini na inaendelea kuchapa kazi kwa lengo la kutatua
changamoto zinazowakabili wananchi kwenye maeneo mbalimbali nchini
yakiwemo na mkoa wa Morogoro.
Pia,
Waziri Mkuu alisema kila mtumishi wa umma anatakiwa ahakikishe anafanya
kazi kwa bidii ili kuiwezesha Serikali kutimiza lengo lake la kuboresha
maendeleo ya wananchi kwenye maeneo mbalimbali nchini hususani ya
vijijini.
Waziri
Mkuu alisema iwapo watumishi wa umma watatimiza majukumu yao ipasavyo
changamoto nyingi zinazowakabili wananchi kama upatikanaji wa maji
zitakuwa historia kwa kuwa Serikali inatoa fedha nyingi kwa ajili ya
utekelezaji wa miradi hiyo.
Alisema
watumishi wa umma wanapaswa kuwa na nidhamu ya fedha za Serikali
zinazopelekwa katika maeneo kwa ajili ya kugharamia miradi ya maendeleo
ikiwemo ya afya, elimu na maji. “ Sina mzaha na watakaotafuna fedha
hizo.”
EmoticonEmoticon
Note: Only a member of this blog may post a comment.