NA.MWANDISHI
WETU
WADAU wa masuala ya Wanawake na Watoto
wamekutana ili kujadili na kufanya tathimini ya Utekelezaji wa Mpango Kazi wa
Taifa wa Kutokomeza Ukatili Dhidi ya Wanawake na Watoto (MTAKUWWA) kwa kipindi
cha robo ya kwanza 2019/2020.
Akizungumza wakati akifungua kikao
kazi hicho cha siku mbili kuanzia Septemba 18 hadi 19, 2019 kilichofanyika katika
Ukumbi wa Bwalo la JKT UMWEMA mkoani Morogoro Mratibu wa Taifa wa Mpango huo
Bi. Happiness Mugyabuso amesema, Serikali kwa kushirikiana na Washirika wa
Maendeleo wameandaa kikao kazi hicho ili kujadili na kufanya tathimini ya
utekelezaji wa Mpango Kazi huo.
“Leo tumekutana hapa kwa pamoja kwa lengo la
kufanya tathimini ya utekelezaji wa mpango kazi huo katika kipindi cha robo ya
kwanza kwa Mwaka 2019/2020. Aliongezea kuwa, pamoja na mafanikio yaliyopatikana
katika robo ya kwanza ya utekelezaji wa Mpango Kazi, kikao kazi kitajadili pia
changamoto zilizojitokeza katika kipindi husika na kuweka mikakati mahsusi ya
kuimarisha utekelezaji wake kwa vipindi vya robo zinazofuata,”alisema Bi.
Happiness.
Aidha
kikao hicho kilitoa fursa ya kujadili namna bora ya kuboresha mfumo wa
ukusanyaji na uchakataji wa taarifa za takwimu za utekelezaji wa MTAKUWWA ili
kuimarisha upatikanaji wa takwimu za msingi (baseline
data). Hatua hii ni muhimu kwani itasaidia kupima hali ya utekelezaji wa
Mpango Kazi katika vipindi mbalimbali vikiwemo vya mwaka na miaka mitano (5).
Mmoja
wa washiriki wa kikao hicho Bw.Emmanuel Burton ambaye ni Afisa Maendeleo ya
Jamii kutoka Idara kuu ya Maendeleo ya Jamii alieleza kuwa, Miongoni mwa maeneo
yaliyojadiliwa ni pamoja na namna bora ya upatikanaji wa taarifa sahihi za
utekelezaji katika sekta mbalimbali ambazo zinatekeleza mpango huo na kuwa na
mikakati ya namna ya kuwafikia walengwa kikamilifu ili kukidhi lengo mpango
ifikapo mwaka 2021/ 2022.
“Kikao
kazi hiki ni muhimu kwa kuzingatia kuwa, malengo mahsusi ya utekelezaji wa
Mpango wa MTAKUWWA yanajadiliwa na kuhakikisha tunaandaa taarifa sahihi zenye
tija kuhusu makundi hayo ili vita dhidi ya ukatili wa wanawake na watoto
inapiganwa na kuleta matokeo chanya,”alisema Burton
Konstebo wa Polisi Bi. Tunu
Mohamed akieleza kuhusu takwimu za madawati ya jinsia na watoto yaliyopo katika
vituo vya polisi nchini wakati wa kikao
kazi hicho.
|
Afisa Maendeleo ya Jamii
kutoka Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto Bi.Juliana Tarimo
akifafanua jambo wakati wa kikao kazi hicho.
|
Afisa Takwimu Munir Mdee
kutoka Ofisi ya TAKWIMU akifafanua jambo kuhusu masuala ya takwimu wakati wa
kikao hicho.
|
Bi. Juliana Ntukey akiongoza
majadiliano katika kazi za vikundi wakati wa kikao kazi hicho.
|
EmoticonEmoticon
Note: Only a member of this blog may post a comment.