Monday, September 16, 2019

SERIKALI YACHUKIZWA NA MGONGANO WA DC, DED MALINYI


        *Waziri Mkuu aelekeza weledi wao kiutendaji uchunguzwe

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amechukizwa na mgongano uliopo kati ya Mkuu wa Wilaya ya Malinyi, Majura Kasika na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya wilaya hiyo Mussa Mnyeti, hivyo kumuelekeza Mdhibiti na Mkaguzi wa Hesabu za Serikali (CAG) na Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Utumishi na Utawala Bora kwenda kuchunguza weledi wa utendaji kazi  wao.

“Ni aibu Mheshimiwa Rais Dkt. John Magufuli amewateua vijana wawe viongozi lakini leo hadi wananchi wa kawaida wanajua mgongano wenu maofisini. Ni aibu Mkuu wa Wilaya ya Mkurugenzi mnagombana tena wakati mwingine mnagombania miradi, mmesahau kutekeleza majukumu yenu.”

Waziri Mkuu ametoa maelekezo hayo leo (Jumatatu, Septemba 16, 2019) wakati akizungumza na watumishi wa wilaya ya Malinyi pamoja na wananchi katika mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye uwanja wa Toboa, akiwa katika siku ya tatu ya ziara yake ya kikazi mkoani Morogoro.

Amesema Serikali imewapa nafasi hiyo ili wakasimamie maendeleo ya wananchi na inapeleka fedha kwa ajili ya kuboresha maendeleo ya jamii kama kuimarisha huduma za afya, elimu, maji na miundombinu ya barabara lakini wao wanagombania miradi na mingine wanaichakachua.

Waziri Mkuu amesema mbali na CAG na Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Utumishi na Utawala Bora kwenda kuchunguza utendaji wa viongozi hao, pia ameuelekeza uongozi wa Wakala wa Majengo Tanzania (TBA) wakakague miradi ya ujenzi inayotekelezwa kwenye wilaya hiyo kama ubora wake unalingana na thamani halisi.” Baada ya kupata majibu ya uchunguzi na kubaini kiini cha tatizo ndani ya wilaya hii hatua zitachukuliwa.”

Awali, Mbunge wa Jimbo la Malinyi, Dkt. Haji Mponda alimweleza Waziri Mkuu kwamba kwenye wilaya hiyo kuna matatizo ya mahusiano kati ya Serikali na Halmashauri jambo linalosababisha kukwama kwa shughuli za maendeleo.

Mbunge huyo alisema kutoelewana kwa viongozi wa wilaya hiyo Mkuu wa Wilaya na Mkurugenzi kumesababisha mgawanyo mkubwa kuanzia katika Baraza la Madiwani hadi kwa wananchi mitaani, hivvyo alimuomba Waziri Mkuu awasaidie katika. Kilipatia ufumbuzi suala hilo.

Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu  amesema kuwepo kwa mabango mengi kwenye mikutano ya hadhara  ya viongozi wakuu kunadhihirisha wazi kwamba watendaji wa Halmashauri hawawatembelei  wananchi katika maeneo yao na kutatua kero mbalimbali zinazowakabili.

“Watendaji hamuendi kuwatembelea wananchi na kusikiliza matatizo yao, haiwezekana wawe wanawasubiri viongozi wa juu na kuwasilisha kero zao kwa njia ya mabango, sasa jipangeni haya mabango yote mtakuja kuyajibu kwa sababu katika mabango yao hakuna hoja hata moja inayomuhusu Waziri Mkuu zote ni za ngazi ya halmashauri.”

Waziri Mkuu amesema Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Rais Dkt. John Magufuli imeelekeza nguvu kubwa katika kuwatumikia wananchi na kutatua kero zao, hivyo itasimamia kuhakikisha kila mtumishi anawajibika kwa kiwango kinachostahili.

Mapemaalipowasili wilayani Malinyi, Waziri Mkuu aliweka jiwe la msingi la ujenzi wa jengo la ofisi ya Halmashauri ya Wilaya ya Malinyi linalojengwa na Shirika la Nyumba la Taifa kwa gharama ya sh. bilioni 3.9. Ujenzi huo ulianza 29/11/ 2017 na utakamilika 29/09/ 2019. 


 (mwisho)


EmoticonEmoticon

Note: Only a member of this blog may post a comment.