Monday, September 16, 2019

SERIKALI KUENDELEA KUJUMUISHA MASUALA YA WATU WENYE ULEMAVU KATIKA MIPAGO NA BAJETI NGAZI YA WIZARA

Serikali kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Ajira, Vijana na Watu wenye Ulemavu) imewahakikishia watu wenye ulemavu nchini kupitia Shirikisho la Watu wenye Ulemavu Tanzania (SHIVYAWATA) kuwa itaendelea kujumuisha masuala ya watu wenye ulemavu katika mipango na bajeti kwa ngazi ya Wizara ili kuweza kuhakikisha watu wenye ulemavu wanapata huduma bora  na stahiki.

Akiongea wakati wa kikao kazi  kuhusu ushawishi na utetezi pamoja na ujumuishwaji wa  masuala  ya watu wenye ulemavu katika mipango na bajeti  ngazi ya wizara,  kilicho washirikisha Menejimenti ya Ofisi ya Waziri Mkuu, viongozi kutoka SHIVYAWATA na Shirika la Kimataifa la ADD, leo jijini Dodoma, tarehe 16 Septemba, 2019, Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Watu wenye Ulemavu wa Ofisi hiyo, Filbert Kawemwamwa amebainisha kuwa lengo la kikao hicho  ni kuibua mikakati ya ujumuishaji, usimamizi na utekelezaji wa masuala watu wenye ulemavu nchini.

“Katika kuhakikisha kuwa mipango na bajeti ngazi ya wizara zinajumuisha masuala ya watu wenye ulemavu tutaendelea kukutana na wizara nyingine saba za kisekta ili kuweza kuhakikisha mipango ya maendeleo yao inaweza kuwafikia watu wenye ulemavu hasa walio vijijini, kwa kuzingatia Sera ya Taifa ya Maendeleo na Huduma ya  Watu wenye Ulemavu ya Mwaka 20014” amesistiza Kawemwamwa

Awali akiongea katika kikao hicho Mwenyekiti wa Shirikisho la Watu wenye Ulemavu Tanzania (SHIVYAWATA), Ummy Nderiananga, ameshukuru kwa jitihada zinazofanywa na serikali ya awamu ya Tano, inayoongozwa na Dkt. John Pombe Magufuli katika kuboresha huduma za msingi za watu wenye Ulemavu nchini, hata hivyo amebainisha kuwa wanazo hoja za msukumo kumi ambazo anaamini utekelezaji wake ukikamilika zitaboresha huduma  na maendeleo kwa watu wenye ulemavu nchini.

“Tayari serikali kupitia ofisi ya Waziri Mkuu imeshaunda madawati ya watu wenye ulemavu katika wizara na taasisi zake tunaomba majukumu ya maofisa hao yapitiwe upya, pia uanzishwaji wa mchakato wa uundwaji wa mfuko wa Kitaifa wa watu wenye Ulemavu, masuala mengine ni kuanzishwa kwa rejista  ya watu wenye ulemavu, kupitia sheria ya watu wenye ulemavu, Makakati wa ufukiwaji wa 3% ya watu wenye ulemavu kwenye kila taasisi inayo ajiri watu kuanzia 20”  amesema Nderiananga

Ameongeza kuwa wanaomba serikali isisimamie ukamilishwaji wa mchakato wa uandaaji wa taarifa ya utekelezaji wa mkataba wa umoja wa mataifa  wa haki za watu wenye Ulemavu, pamoja na kuwaelekeza waajiri wote kuandaa na kuwasilisha taarifa ya mwaka ya hali ya ajira  kwa watu wenye ulemavu katika taasisi zao, pia ukamilshawaji wa mwongozo wa viwango vya ufikikaji wa miundo mbinu, Mipango ya Kisekta pamoja na Baraza la ushauri la watu wenye ulemavu kuhakikisha  linafanya kazi kikamilifu.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Programu, Shirika la Kimataifa la ADD, Rose Tesha, amefafanua kuwa shirika hilo limeamua kuunga juhudi za serikali za kuwahudumua watu wenye Ulemavu kwa kuwezesha SHIVYAWATA kukutana na wizara za kisekta ili kuweza kuhakikisha kuwa wanaweza kuzitetea vizuri fursa na haki za watu wenye ulemavu hapa nchini.

Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Ajira, Vijana na Watu wenye Ulemavu) iliundwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Tangazo  kwenye gazeti la Serikali Na.144 la mwezi Aprili, 2016. Pamoja na majukumu mengine Ofisi hiyo inajukumu la kusimamia utekelezaji wa sera, sheria, AMiongozo, Kanuni na Viwango vya Ubora katika utoaji wa huduma za watu wenye ulemavu nchini.
MWISHO.


EmoticonEmoticon

Note: Only a member of this blog may post a comment.