*Amwagiza Mkuu wa Mkoa aungalie vizuri mkoa wake
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amemsimamisha kazi Mhandisi wa Ujenzi wa wilaya ya Morogoro, Brown Undule baada ya kushindwa kutekeleza majukumu yake ipasavyo, ikiwemo usimamizi mbovu wa ujenzi wa kituo cha afya Mkuyuni.
Amemsimamisha kazi Mhandisi huyo leo (Jumatano, Septemba 18, 2019) baada ya kukagua ujenzi wa kituo hicho cha afya akiwa katika siku ya tano ya ziara yake ya kikazi mkoani Morogoro. Amesema hajaridhishwa na aina ya milango iliyotumika.
“Milango yote katika jengo hili ing’olewe leo leo, huwezi kuweka milango ya hovyo namna hii yaani mtu wa nje anamuona aliyeko ndani, nimesitisha kuendelea kukagua jengo. Yeye na usomi wake ameridhishwa na milango ya hovyo kama hii.”
Waziri Mkuu amesema aina ya milango iliyowekwa katika kituo hicho cha afya haiwezi kutumika hata kwenye nyumba ya mtu binafsi, lakini kutokana na uangalizi mbovu kutoka kwa watendaji walikubali kuweka milango hiyo mibovu.
Amesema Serikali imeamua kujenga vituo vya afya vitano kwenye wilaya hiyo ili kusogeza huduma za afya kwa wananchi na kuwapunguzia kutembea umbali mrefu kufuata huduma za afya, hivyo amewataka watendaji wasimamie ipasavyo miradi hiyo.
Amesema Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Rais Dkt. John Magufuli imedhamiria kuboresha huduma za afya kwa wananchi, hivyo amewataka wananchi hao waendelee kuwa na imani na Serikali yao.
Baada ya kukagua ujenzi wa kituo hicho cha afya, Waziri Mkuu amekagua ujenzi wa hospitali ya wilaya, ambako nako ameagiza kuong’olewa kwa mbao zote zilizotumika kwa ajili ya kupaulia jengo la mama na mtoto la hospitali hiyo kwa kuwa hazina viwango. “Fundi usiendelee na kazi hii ya upauaji kwa sababu mbao unazotumia hazikidhi viwango.”
Kwa upande wake, fundi anayejenga jengo hilo la mama na mtoto, Johnson Ishengoma amesema changamoto kubwa anayoipata katika ujenzi huo ni ucheleweshwaji wa vifaa pamoja na kulazimishwa kutumia vifaa vilivyo chini ya kiwango.
Fundi huyo ametolea mfano suala la mbao za kupaulia kuwa aliomba mbao za urefu wa futi 20 lakini aliletewa mbao zenye urefu wa futi 12 na kulazimishwa azitumie hivyo hivyo. “Mhandisi wa wilaya Brown Undule na mtu wa manunuzi Grace ndio wanaoniletea vifaa hivi. Baadhi ya vifaa huwa navikataa kutokana na kutokuwa na ubora.”
Katika hatua nyingine,Waziri Mkuu amemuagiza Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Dkt. Steven Kebwe kuuangalia vizuri mkoa wake na kuhakikisha anauchunga vizuri kwa sababu umekithiri kwa matumizi mabaya ya fedha za umma.
“Wakati nikiendelea na ziara mkoani hapa, nimepata taarifa kwamba zaidi ya sh.milioni tisa zimetumika kwa ajili ya kilipana posho katika Halmashauri ya mji Ifakara . Posho hizo ni kwa ajili ya ziara ya Waziri Mkuu na imetoka kwa mtendaji wa kata ya Viwanja 60, hili jambo halikubaliki. Nakukabidhi risiti zote na uwachukulie hatua wote waliohusika. Mkoa wa Morogoro ni shida”
Wakingumzia kuhusu utendaji wa Serikali ya Awamu ya Tano na ujenzi wa miradi ya maendeleo inayotekelezwa katika maeneo yao, wakazi wa Tarafa ya Mkuyuni wameipongeza Serikali kwa namna inavyowajali wananchi wake ikiwa ni pamoja na kuboresha huduma.
Mmoja wa wananchi hao, Uwesu Mwichumu (71) mkazi wa kijiji cha Kibungo ameipongeza Serikali kwa usimamizi wa miradi na hatua inazochukua kwa baadhi ya watendaji wanaojihusisha na wizi wa fedha za umma.
Amesema Serikali inajitahidi kuwaletea miradi ya maendeleo kwenye maeneo yao tatizo lililopo ni kwa watendaji wa chini. “Watendaji wengi huku chini wanashindwa kutekeleza majuku yao ipasavyo, wanashirikiana na wazabuni kuiibia Serikali.”
Mkazi mwingine wa Tarafa hiyo, Hanifa Shaban amesema anaishukuru Serikali kwa kuboresha huduma mbalimbali ikiwemo upatikanaji wa dawa katika vituo vya afya na zahanati. Amesema awali walikuwa wanakwenda zahanati na kuandikiwa vyeti bila ya kupewa dawa , hivyo walilazimika kwenda kununua kwenye maduka ya dawa jambo ambalo kwa sasa halipo.
(mwisho)
EmoticonEmoticon
Note: Only a member of this blog may post a comment.